Kupiga Kura
Ibara ya 5 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imempa haki kila raia aliyetimiza umri wa miaka kumi na minane kupiga kura.Kwa mujibu wa vifungu vya 81 (1) na (2) na 85 (1) vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, ili mtu aweze kupiga kura anatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:-
(i) Awe ni raia wa Jamhuri ya Muungano:
(ii) Awe amejiandikisha katika Daftari la kudumu la wapiga kura :
(iii) Awe amejiandikisha katika Jimbo au Kata; na
(iv) Awe katika kituo alichopangiwa katika eneo la uchaguzi ambalo amejiandikisha kama mpiga kura.
Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani inamruhusu mtu kupiga kura kwa kufuata utaratibu ufautao:
(i) Mpiga Kura anatakiwa kwenda kwenye kituo cha kupigia kura alichojiandikisha akiwa na kadi yake ya kupigia kura.
(ii) Mpiga kura anatakiwa kupanga mstari akiwa kituo cha kupigia kura na kusubiri hadi zamu yake ya kupiga kura itakapowadia.
(iii) Mpiga kura anatakiwa afuate maelekezo yote atakayopewa na msimamizi wa kituo muda wote akiwa kituoni.
(iv) Baada ya kumaliza kupiga kura, mpiga kura anatakiwa kurudi nyumbani.