Uwekaji Wazi Daftari la Awali
Uwekaji Wazi Daftari la Awali
Kwa mujibu wa Kifungu cha 24 (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, Afisa mwandikishaji ataweka wazi Daftari la Awali la Wapiga Kura katika kila kata na, ikilazimu, anaweza kufanya marekebisho kwa namna itakavyoelekezwa na Tume. Aidha Kifungu cha 34 cha Kanuni za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura za Mwaka 2024, Tume au Mkurugenzi wa Uchaguzi, afisa mwandikishaji ataweka au kuwezesha kuwekwa wazi kwa Daftari la Awali la Wapiga Kura kwa kila kata kwa ajili ya kukaguliwa na umma katika muda utakaoamuliwa na Tume. Tume huweka wazi Daftari la Awali la Wapiga Kura ili kutoa fursa kwa wananchi:
- Kulikagua Daftari;
- Kufanya marekebisho ya majina au mahali wanapoishi;
- Kuingiza au kufuta majina ya Wapiga Kura;
- Kuweka pingamizi kwa Mpiga Kura aliyeandikishwa na hana sifa za kuwemo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Kumuwekea Pingamizi aliyeandikishwa kwenye Daftari la Awali
Kwa mujibu wa Kifungu cha 26 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, Mtu ambaye jina lake lipo katika Daftari la Awali la Wapiga Kura la eneo lolote la uchaguzi anaweza kupinga kuendelea kuwemo kwa jina lake mwenyewe au jina la mtu mwingine yeyote katika Daftari la Awali la Wapiga Kura kwa sababu yeye au mtu huyo mwingine hana sifa au amepoteza sifa za kuandikishwa au mtu huyo mwingine amefariki. (2) Mtu anayeweka pingamizi chini ya kifungu hiki atajulikana kama “mweka pingamizi”
Kifungu cha 27(1), (2) na (3) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, kila pingamizi litawekwa kwa kujaza nakala mbili za fomu iliyoainishwa na litawasilishwa kwa afisa mwandikishaji ndani ya muda ulioainishwa. Kila pingamizi, litawasilishwa likiambatishwa na malipo ya dhamana ya kiasi cha fedha kitakachoainishwa na Tume kwa notisi itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali. Afisa mwandikishaji, mapema iwezekanavyo baada ya kupokea pingamizi lililowekwa kwa mujibu wa Sehemu hii, atapeleka taarifa ya pingamizi hilo kwa mtu aliyewekewa pingamizi: Isipokuwa kwamba, afisa mwandikishaji atapaswa kubandika taarifa ya pingamizi katika mbao za matangazo katika kituo cha uandikishaji endapo pingamizi limewekwa kwa sababu mtu ambaye jina lake limo katika Daftari la Awali la Wapiga Kura amefariki.
Kifungu cha 29 (1) na (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, endapo mweka pingamizi au mtu aliyewekewa pingamizi hataridhika na uamuzi wa afisa mwandikishaji chini ya kifungu cha 28, mweka pingamizi au mtu huyo anaweza, ndani ya siku saba tangu tarehe ya uamuzi huo kutolewa, kukata rufaa katika Mahakama ya Mwanzo. Mahakama ya Mwanzo itatoa uamuzi wa rufaa ndani ya siku kumi na nne tangu siku rufaa ilipowasilishwa.