Historia ya Tume
Mwaka 1991, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Ali Hassan Mwinyi aliteua Tume chini ya Uenyekiti wa Hayati Jaji Mkuu Mstaafu Francis Nyalali. Madhumuni ya Tume hiyo ilikuwa ni kukusanya maoni ya wananchi juu ya kuendelea na mfumo wa chama kimoja au kuwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa. Kutokana na ripoti ya Tume hiyo, ibara ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ilirekebishwa na kufanya Tanzania kuwa Taifa linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Vilevile, Sheria ya Vyama vya Siasa, (Na. 5 ya 1992) ilitungwa ili kuwezesha usajili wa vyama vya siasa. Pia, Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, (Na.1 ya 1985) na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, (Na. 4 ya 1979) zilirekebishwa ili kuondokana na mfumo wa chama kimoja na kuruhusu kufanyika kwa Uchaguzi chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa. Baada ya marekebisho hayo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilianzishwa tarehe 13 Januari, 1993.
Aidha, mwaka 2021 ulifanyika Mkutano wa Wadau wa Kujadili Hali ya Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa nchini Tanzania. Pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulitoka na azimio la kuboresha mfumo wa uchaguzi nchini. Hivyo, tarehe 23 Desemba 2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda kikosi kazi cha kutathmini hali ya demokrasia ili kutoa mapendekezo ya kuboresha masuala ya demokrasia na hali ya kisiasa nchini.
Kikosi kazi, kilitoa mapendekezo ya kufanyika kwa maboresho ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292. Maboresho hayo yalisababisha kutungwa kwa Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024 na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024. Kufuatia kutungwa kwa Sheria hizo, jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi lilibadilika na kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imeanzishwa kwa mujibu wa ibara ya 74(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Kwa kuzingatia masharti ya ibara ya 74(7) na (11) ya Katiba na kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024, Tume ni idara huru inayojitegemea na inafanya maamuzi yake rasmi kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kwa vikao. Katika kutekeleza majukumu yake ya kikatiba, Tume haitalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote au idara yoyote ya Serikali au maoni ya chama chochote cha siasa.