INEC yatoa elimu kwa Ma-OCD nchini kuhusu sheria za uchaguzi
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) katika kuhakikisha inatoa Elimu ya Mpiga Kura kwa makundi mbalimbali katika jamii, imetoa elimu hiyo kwa Wakuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) nchini katika mafunzo yaliyofanyika katika Shule ya Polisi Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza mara baada ya mafunzo hayo ya siku moja kuhusu Sheria mbalimbali na Kanuni zinazoiongoza Tume, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani amesema kwa kuwapa elimu hiyo maafisa hao wa Polisi ngazi ya Wilaya kutasaidia kuondoa migongano baina yao na Vyama vya siasa.
“Kimsingi hawa ndio wasimamizi wa sheria ngazi ya Wilaya kutoka Jeshi la Polisi, hivyo tumewapitisha katika Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024 na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 ili waweze kuzitafsiri vyema sheria hizo na kusimamia vyema majukumu yao bila kuleta mtafaruku kwa chama cha siasa au na wananchi kwa ujumla,” alisema Bw. Kailima.
Kailima amesema kwa sasa Polisi wanajua wajibu wao ni nini katika kutekeleza yao na chama cha siasa kinatakiwa kufanya nini wakati huu ambapo Tume inaendelea na zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini.
Aidha, Kailima amesema wakati wa kuelekea uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, Tume itakutana tena na Jeshi hilo na kuwapa ufafanuzi juu ya mambo mbalimbali yanayohusu Uchaguzi Mkuu ili kuendelea kuwa na uchaguzi mkuu wa amani, huru na haki.
Kwa upande wake Kamishna wa Operesheni na Mafunzo Jeshi la Polisi, CP Awadhi Juma Haji amesema lengo la mafunzo hayo ni kuliweka tayari Jeshi la Polisi wakati wa mchakato wa uchaguzi na kwa kuzingatia kuwa wao ndio wasimamizi wa sheria na walinzi wa raia na mali zao wakati wote.
CP Awadhi amesema Tume imewapa elimu juu ya wajibu wa Polisi katika shughuli za uchaguzi, sheria na kanuni mbalimbali wakati huu wa uboreshaji na lengo ni kujipanga na kuhakikisha mazoezi yanayoendelea nchini yanafanyika katika hali ya usalama.
Mafunzo hayo ya siku nne ya Wakuu wa Polisi Wilaya Nchini yaliyoanza Novemba 4, 2024 yamefikia tamati Novemba 8 mwaka huu ambapo mada mbalimbali kuhusu uchaguzi na ushiriki wa jeshi la Polisi zimetolewa.