Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Mwenyekiti wa INEC, Mhe. Jacobs Mwambegele ashuhudia uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Kwahani, asema umekwenda vizuri

Imewekwa: 08 Jun, 2024
Mwenyekiti wa INEC, Mhe. Jacobs Mwambegele ashuhudia uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Kwahani, asema umekwenda vizuri

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele ameshuhudia wananchi wa Jimbo la Kwahani Mkoa wa Mjini Magharibi wakipiga kura katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo kumchagua Mbunge wao.

Jaji Mwambegele aliambatana na Mjumbe wa Tume hiyo, Mhe. Dkt. Zakia Mohamed Abubakar ambapo walitembelea vituo hivyo vya kupigia kura na kushuhudia ufunguaji wa vituo  saa moja kamili asubuhi.

Akizungumza baada ya kutembelea vituo vya kupigia kura katika Skuli ya Sebleni, Uwanja wa Negro na Kariakoo, Jaji Mwambegele alisema zoezi linakwenda vizuri na wao walishuhudia vituo vikifunguliwa kwa wakati na wananchi kupiga kura.

Aidha, amesema vyama vya siasa vimeweka mawakala wakutosha katika katika vituo vyote vya kupigia kura walivyotembelea.

“Tumeshuhudia ufunguzi wa vituo na upigaji kura, vituo vimefunguliwa kwa wakati na wananchi wamejitokeza kwa wingi kuja kutumia haki yao ya kupiga kura pia vyama vya siasa vimeweka mawakala wakutosha katika vituo hivyo,”alisema Jaji Mwambegele.

Jaji Mwambegele amesema wananchi wa Jimbo la Kwahani wameonesha mwitikio mkubwa kwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuchagua kiongozi wanayemtaka.

Vyama 14 vimesimamisha wagombea katika Uchaguzi huo mdogo wa kiti cha Ubunge jimbo la Kwahani ambapo majina yao na vyama katika Mabano ni Bw.  Bashir Yatabu Said (Demokrasia Makaini), Bi. Nuru Abdulla Shamte (DP), Bi. Mwanakombo Hamad Hassan (NLD), Bi. Zainab Maulid Abdallah (CCK), Bi. Tatu Omary Mungi (UPDP), Bw. Khamis Yussuuf Mussa (CCM) na Bi. Jarade Ased Khamis (AAFP).

Wengine ni  Bw. Kombo Ali Juma (NRA), Bi. Shara Amran Khamis (ADC), Bi. Naima Salum Hamad (UDP), Bi. Madina Mwalim Hamad (ADA TADEA), Bw. Amour Haji Ali (SAU), Bi. Mashavu Alawi Haji (UMD) na Bw. Abdi Khamis Ramadhan (CUF).