Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi awataka watendaji wa vituo vya uboreshaji wa Daftari Arusha kuzingatia mafunzo

Imewekwa: 09 Dec, 2024
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi awataka watendaji wa vituo vya uboreshaji wa Daftari Arusha kuzingatia mafunzo

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele amewataka waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya bayometriki wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha na Jiji la Arusha kuzingatia mafunzo ili kufanikisha uboreshaji wa Daftari.

Mhe. Jaji (Rufaa) Mwambegele ameyasema hayo wakati wa mafunzo kwa waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya bayometriki wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha na Jiji la Arusha, ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari unaotarajiwa kuanza tarehe 11 Desemba, 2024.

Amesema lengo la yeye kwenda kutembelea mafunzo hayo ni kuangalia jinsi mafunzo yanavyofanyika na amewasihi washiriki hao wa mafunzo wasisite kuuliza maswali pale penye changamoto ili waweze kufahamu vyema mafunzo na kutekeleza jukumu lao kwa mafanikio.

“Kama kuna changamoto hapa kwenye mafunzo mtaziwasilisha kwa viongozi wenu kwani Tume inawategemea nyinyi kufanikisha zoezi la uboreshaji wa Daftari” amesema Mhe Jaji (Rufaa) Mwambegele na kuongeza:.

“Sasa naombeni wote mzingatie mafunzo haya kwa sababu utendaji mzuri wa kazi wa Tume unawategemea nyinyi, nyinyi mkifanya kazi vizuri, Tume inasifiwa kwamba imefanya kazi vizuri kwa hiyo tusifanye kazi kwa kubahatisha”

Amefafanua kuwa kutokana na  mafunzo yanavyofanyika kwa wakufunzi kuwafundisha na kuwakumbusha jinsi ya kutekeleza zoezi hilo, ana hakika kwamba Mkoa wa Arusha mambo yatakwenda vizuri.

Hivyo, Mhe. Jaji (Rufaa) Mwambegele amewatakia mafunzo mema waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya bayometriki hao kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Arusha na Jiji la Arusha wapatao 600 na hatiamaye kazi njema kwenye vituo vya uboreshaji wa Daftari.

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura upo katika mzunguko wa saba unaohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Kondo na Mji wa Kondoa katika Mkoa wa Dodoma kuanzia tarehe 11 hadi 17 Desemba, 2024.

Ubireshaji huo ulizinduliwa rasmi mkoani Kigoma mnamo tarehe 20 Julai, 2024 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na kuendelea katika mikoa mingine.

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wa Mwaka 2024/2025 unakwenda na Kaulimbiu inayosema “Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura Ni Msingi wa Uchaguzi Bora”.