Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (Rufaa) Mhe. Jacobs Mwambegele awakumbusha watanzania wakikosa kujiandikisha au kuboresha taarifa watakosa haki ya kuwachagua viongozi wao

Imewekwa: 19 May, 2025
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (Rufaa) Mhe. Jacobs Mwambegele awakumbusha watanzania wakikosa kujiandikisha au kuboresha taarifa watakosa haki ya kuwachagua viongozi wao

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele ametembelea na kukagua mwenendo wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura katika Halmashauri za Wilaya ya Bagamoyo na Chalinze  Mkoa wa Pwani.

Akizungumza na Uchaguzi Online Tv baada ya kukagua zoezi hilo, Mhe. Mwambegele amewataka wananchi ambao bado hawajajiandikisha kwenye Daftari watumie fursa ya siku zilizobaki kwenda kujiandikisha au kuboresha taarofa zao ili waweze kutimiza haki yao ya kupiga kura wakati wa uchaguzi.

Amewasihi watanzania kuwa watumie fursa hiyo kwa sababu baada ya kukamilika kwa uboreshaji wa Daftari Awamu ya Pili na Uwekaji Wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura tarehe 22 Mei, 2025 hakutakuwa na uboreshaji mwingine wa Daftari.

“Wananchi tafadhali tunaomba mjitokeze mjiandikishe au kuboresha taarifa zenu, usipojitokeza kuja kujiandikisha au kuboresha taarifa zako uwe na uhakika kwamba hutashiriki katika kuchagua kiongozi wako inapofika wakati wa uchaguzi”, amesema Mhe. Mwambegele.

Mhe Mwambegele amesema  wajumbe wengine wa Tume Huru ya  Taifa ya Uchaguzi wapo kwenye halmashauri mbalimbali za mikoa 16 ya Tanzania Bara na Zanzibar inayoshiriki katika uboreshaji wa Daftari katika mzunguko wa pili na wamekagua mwenendo wa uboreshaji wa Daftari na kwamba zoezi linakwenda vizuri.

Awamu ya Pili ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na Uwekaji Wazi wa daftari la Awali la Wapiga Kura imeanza tarehe 16 hadi 22 Mei, 2025 ikihusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Dodoma, Manyara, Singida, Tanga, Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba.