Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan atoa wito kwa watanzania kuwa wazalendo kwa kujitokeza kwenda kujiandikisha

Imewekwa: 18 May, 2025
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan atoa wito kwa watanzania kuwa wazalendo kwa  kujitokeza kwenda kujiandikisha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa watanzania kuwa wazalendo kwa kutumia fursa ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kujitokeza kwenda kujiandikisha au kuboresha taarifa zake.

Mhe.Samia ameyasema hayo baada ya kwenda kuboresha taarifa zake kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye kituo cha Kuandikisha Wapiga Kura kilichopo kilichopo Ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Chamwino Mkoa wa Dodoma.

Amesema kujiandikisha ni fursa kubwa inatokea kila baada ya miaka mitano haiji kila siku kwa hiyo, ametoa wito ni vyema kila mtanzania ajitokeze atumie fursa hiyo

Amesema kutokujitokeza kujiandikisha ni kukataa mwenyewe haki yako ya kikatiba na Mtanzania anapokataa haki yake ya kikatiba ajitafakari uzalendo wake, je ni mzalendo.

“Ni mzalendo wa aina gani ambaye katiba imekupa fursa nenda kajiandikishe, piga kura chagua kiongozi unayehisi atakuja kukuhudumia, wewe unaikataa” amehoja Mhe. Samia na kuongeza:

“Ukiikataa haki yako (ya kuchagua kiongozi) wenzio watakwenda kuweka (kiongozi) wanayemtaka, kwa hiyo wewe utabaki kulalamika. Lakini suala kubwa ni uzalendo jiulize mwenyewe uzalendo wangu uko wapi’”

“Hii ni fursa kubwa inatokea kila baada ya miaka mitano haiji kila siku kwa hiyo ni vyema kila mtanzania na huo ndio wito wangu kila mtanzania ajitokeze atumie fursa hii.

Awamu ya Pili ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na Uwekaji Wazi wa daftari la Awali la Wapiga Kura imeanza tarehe 16 hadi 22 Mei, 2025 ikihusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Dodoma, Manyara, Singida, Tanga, Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba.