Spika Dkt, Tulia azitaka taasisi za haki jinai kuiunga mkono mahakama ili kuharakisha zaidi upatikanaji wa haki

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb) amezitaka taasisi za haki jinai kuangalia uwezekano wa kutumia mfumo mpya wa Kielektroniki wa Kusimamia Kesi ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa haraka zaidi kwa wananchi.
Dkt. Tulia ameyasema hayo wakati akizindua Wiki ya Sheria na mfumo huo katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.
Alisema suala la utoaji haki si la mahakama pekee na kwamba mahakama inatarajia kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa mawakili na wadau wengine wa haki jinai ili wananchi wapate haki kwa haraka na inayostahili.
“Kaulimbiu ya siku ya sheria ni “Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa taifa: Nafasi ya Mahakama na wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa haki jinai”, alisema Dkt. Tulia na kuongeza:
“Kaulimbiu hii inaashiria kwamba mfumo wa utoaji haki si wa mahakama peke yake, mahakama inawatarajia mawakili wawe sehemu ya watu ambao watakuwa wanaiongoza mahakama kwenye hoja iliyo mbele yake,
Lakini pia kwenye haki jinai kuna wadau wengi zaidi kama magereza, polisi TAKUKURU na Ofisi ya Mwendesha Mashataka wa Serikali. Ili mahakama iweze kufanya vizuri zaidi na kwa maboresho yote ya Tehama yaliyofanyika, bado wanahitaji kushirikiana na taasisi nyingine.
Kwa hiyo ni muhimu sana taasisi nyingine kwenda na kasi ambayo Mahakama inaenda nayo, kwa hivyo niombe taasisi zote kuangalia namna ambavyo wanaweza kuutumia mfumo huo ili kuisogeza haki kwa haraka zaidi kwa wananchi kwani nia yetu sote ni kwamba mwananchi apete haki kwa haraka na inayostahili.”
Spika Dkt. Tulia aliongeza kuwa kwa kuwa mfumo huo hutumia akili bandia, aliitaka mahakama kujiandaa na kesi za wananchi ambao wameathiriwa na matumizi ya mfumo huo unaotumia akili bandia kwani akili bandia inaweza kutumiwa vibaya na mtu mdanganyifu kwa maslahi yake.
Aidha ameipongeza mahakama kwa kutumia mfumo huo kwani utawawezesha wananchi kupata haki kwa wakati na kwa uwazi zaidi.
Akimkaribisha Spika Dkt. Tulia ambaye alikuwa mgeni rasmi katika usinduzi huo, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamisi Juma alisema mfumo huo utaleta mapiduzi ya uendashaji wa mahakama nchini.
“Tumeambiwa mfumo huu unaotumia akili bandia (artificial intelligence) una mambo mengi mazuri lakini tumeambiwa tuwe na tahadhari. Kwa kutumia mfumo huu badala ya majaji na mahakimu kuwa waandika yale yanayotokea mahakamani kazi ya jaji na hakimu itakua ni kukaa na kusiliza shauri kila kitu kitakuwa tayari na yeye atachagua lugha anayotaka kuitumia.”alisema Jaji Ibrahimu Juma.
Wiki ya Sheria imeanza kuadhimishwa tarehe 24 Januari, 2024 na itahitimishwa tarehe 30 Januari, 2024. Wiki hiyo imeambatana na maonesho ya wadau mbalimbali wa mahakama ikiwemo Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo inashiriki ili kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi katika viwanja vya Nyerere Square.