Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetoa kibali cha uangalizi wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa taasisi na asasi 76 za ndani ya nchi na 12 za kimataifa

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetoa kibali cha uangalizi wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa taasisi na asasi 76 za ndani ya nchi na 12 za kimataifa
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Tume na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Ndg. Ramadhani Kailima vibali hivyo vimetolewa kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 10(1)(i) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024 kikisomwa pamoja na kifungu cha 85(4) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Na. 1 ya Mwaka 2024 na kanuni ya 13(1) na (2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025
Ndg. Kailima amesema Tume, katika kikao chake maalum kilichofanyika tarehe 18 Julai, 2025 imeridhia na kutoa kibali cha uangalizi wa uchaguzi kwa taasisi na asasi 76 za ndani ya nchi na 12 za kimataifa. Orodha ya taasisi na asasi husika inapatikana kupitia tovuti ya Tume ya www.inec.go.tz na mitandao ya kijamii ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 10(1) (g) (h) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024 kikisomwa pamoja na Kanuni ya 22 ya Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za mwaka 2024, katika hicho Tume imeridhia na kutoa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa taasisi na asasi za kiraia 164. Orodha ya taasisi na asasi hizo inapatikana kupitia tovuti ya Tume ya www.inec.go.tz na mitandao ya kijamii ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Taasisi na asasi za kiraia zilizoridhiwa na kupewa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura zitajulishwa kwa njia ya barua pepe kupitia Mfumo wa Usajili (Accreditation Management System) ili kujaza taarifa za kuwawezesha kukamilisha taratibu nyingine ikiwemo kuweka orodha ya watu watakaotoa elimu hiyo.
Kwa upande wa taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kuwa waangalizi wa uchaguzi ziwasilishe kwa njia ya Mfumo wa Usajili (Accreditation Management System) majina ya waangalizi na maeneo waliyopangiwa kufanya uangalizi huo kwa ajili ya kuwaandalia vibali.
Taarifa zingine zote muhimu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya utoaji wa elimu ya mpiga kura na uangalizi wa uchaguzi, miongozo na taratibu zote zitatolewa mapema iwezekanavyo.
Tunazipongeza taasisi na asasi za kiraia ambazo zimepata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura na kuwa waangalizi wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025.
“KURA YAKO HAKI YAKO JITOKEZE KUPIGA KURA”