Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Tume yazialika taasisi na asasi za kiraia kutoa Elimu ya Mpiga Kura katika Uchaguzi Mdogo wa Kata 23

Imewekwa: 12 Apr, 2024
Tume yazialika taasisi na asasi za kiraia kutoa Elimu ya Mpiga Kura katika Uchaguzi Mdogo wa Kata 23

Tume ya Taifa Ya Uchaguzi imekaribisha maombi kutoka taasisi na Asasi za Kiraia nchini zenye nia ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura katika Uchaguzi Mdogo wa Madiwani katika Kata 23 za Tanzania Bara, utakaofanyika siku ya Jumatano tarehe 20 Machi mwaka 2024.

Kata zinazofanya uchaguzi ni Kimbiji iliyopo (Kigamboni Mc), Kasingirima (Kigoma/Ujiji Mc), Ndevelwa (Tabora Mc), Msangani (Kibaha Tc), Utiri (Mbinga Tc), Fukayosi (Bagamoyo Dc), Mlanzi (Kibiti Dc), Mbingamhalule (Songea Dc), Isebya (Mbogwe Dc), Kibata (Kilwa Dc), Mshikamano (Musoma Mc), Na Kata Ya Busegwe Iliyopo (Butiama Dc),

Nyingine ni Kata ya Nkokwa iliyopo (Kyela Dc), Kamwene (Mlimba Dc), Chipuputa (Nanyumbu Dc), Buzilasoga (Sengerema Dc), Mhande (Kwimba Dc), Kabwe (Nkasi Dc), Bukundi (Meatu Dc), Mkuzi (Muheza Dc) na Kata za Boma, Mtimbwani na Mayomboni zilizopo (Mkinga Dc).

Taasisi na Asasi za Kiraia zenye nia ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura zinatakiwa kuwasilisha maombi kwa njia ya barua pepe: Info@Nec.Go.Tz Au Uchaguzi@Nec.Go.Tz

Barua ya maombi inatakiwa kuainisha mambo yafuatayo kuhusu taasisi au asasi husika: -

i. Iwe imesajiliwa kwa mujibu wa Sheria za Tanzania;

ii. Iwe imefanya kazi nchini kwa kipindi kisichopungua miezi sita tangu kusajiliwa kwake;

iii. Ikiwa taasisi au Asasi ya Kiraia inahusisha watendaji wa kimataifa, miongoni mwa watendaji wake wakuu, wawili ambao taarifa zao zitawasilishwa wanapaswa wawe Watanzania;

iv. Katika utendaji wake, iwe haijahusishwa na uchochezi au kuvuruga amani;

v. Iwe na uzoefu wa kutoa Elimu ya Mpiga Kura; na

vi. Iwe tayari kujigharamia katika kutoa Elimu ya Mpiga Kura.

Aidha, maombi yanatakiwa kuambatishwa na: -

i. Nakala au kivuli cha cheti cha usajili;

ii. Nakala au kivuli cha katiba ya taasisi au Asasi ya Kiraia;

iii. Majina matatu ya viongozi wa juu wa taasisi au Asasi ya Kiraia;

iv. Anuani kamili ya makazi na namba za simu za ofisi na viongozi wake; na

v. Ratiba itakayoonesha tarehe na mahali Elimu ya Mpiga Kura itakapotolewa katika halmashauri husika.

Tume haitahusika na utoaji wa rasilimali fedha au rasilimali nyingine kwa ajili ya kugharamia utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura kwa taasisi au Asasi za Kiraia zitakazopewa kibali.

Maombi yatapokelewa kuanzia tarehe 15 hadi tarehe 20 Februari, 2024.