Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Uamuzi wa Pingamizi za Uteuzi wa Wagombea wa Kiti cha Rais kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Imewekwa: 15 Sep, 2025
Uamuzi wa Pingamizi za Uteuzi wa Wagombea wa Kiti cha Rais kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 37 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 kikisomwa pamoja na kanuni ya 22 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025, tarehe 13 Septemba, 2025, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea jumla ya mapingamizi matatu (03) dhidi ya uteuzi wa Ndugu Luhaga Joelson Mpina mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha ACT - Wazalendo na tarehe 14 Septemba, 2025, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea pingamizi moja (01) dhidi ya uteuzi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CСМ).

Tume katika kikao chake kilichofanyika tarehe 15 Septemba, 2025 imefanya uamuzi wa mapingamizi hayo manne (04) yaliyowasilishwa mbele yake, ambapo mapingamizi matatu (03) yamekataliwa na moja (01) limekubaliwa kama ifuatavyo:-

  1. Mapingamizi yaliyokataliwa

Tume imekataa na kuyatupilia mbali mapingamizi matatu (03) kama ifuatavyo:-

i. Pingamizi lililowekwa na Ndugu Almas Hassan Kisabya mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha NRA dhidi ya Ndugu Luhaga Joelson Mpina mgombea wa Kiti cha Rais kupitia Chama cha AСТ Wazalendo.

Tume imekataa na kutupilia mbali pingamizi lililowekwa na Ndugu Almas Hassan Kisabya mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha NRA dhidi ya uteuzi wa Ndugu Luhaga Joelson Mpina kuwa mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.

ii. Pingamizi lililowekwa na Ndugu Kunje Ngomale Mwiru mgombea kiti cha Rais kupitia chama cha AAFP dhidi ya Ndugu Luhaga Joelson Mpina mgombea wa Kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT Wazalendo.

Tume imekataa na kutupilia mbali pingamizi lililowekwa na Ndugu Kunje Ngombale Mwiru mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama AAFP dhidi ya uteuzi wa Ndugu Luhaga Joelson Mpina mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.

iii. Pingamizi lilowekwa na Ndugu Luhaga Joelson Mpina mgombea kupitia Chama cha ACT-Wazalendo dhidi ya Dkt. Samia Suluhu Hassan mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM)

Tume imekataa na kutupilia mbali pingamizi lililowe kwa na Ndugu Luhaga Joelson Mpina dhidi ya uteuzi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).

2. Pingamizi lililokubaliwa

Tume imekubali pingamizi lililowasilishwa na Ndugu Hamza Saidi Johari Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya uteuzi wa Ndugu Luhaga Joelson Mpina kuwa mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha АСТ-Wazalendo.

Hivyo, jina la Ndugu Luhaga Joelson Mpina, mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT- Wazalendo limeondolewa kwenye orodha ya wagombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Imetolewa na:

"KURA YAKO HAKI YAKO JITOKEZE/KUPIGA KURA"

 

Kailima, R. K

MKURUGENZI WA UCHAGUZI