Afisa Mwandikisha wa Jimbo la Kinondoni na Kawe Ndg. Omary Juma atoa wito kwa wakazi wa majimbo hayo kujitokeza kwenda kujiandikisha au kuboresha taarifa zao

Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Kawe na Kinondoni Mkao wa Dar es Salaam Ndg. Omary Juma ametoa wito kwa wananchi wa majimbo hayo kujitokeza kwa wingi kwenda kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiag kura ulioanza leo tarehe 17 Machi, 2025 katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Ndg. Omary ametoa wito huo baada ya kutembelea vituo vya kuandikisha wapiga kura katika majimbo hayo na kushuhudia zoezi la uboreshaji wa Daftari likiendelea vyema ikiwa ni siku ya kwanza.
Amesema baada ya kutembelea vituoni ameshuhudia vituo vya kuandikisha wapiga kura vikifunguliwa mapema saa 2:00 asubuhi na wananchi wakijitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao.
“Katika majimbo ya Kawe na Kinondoni tuna jumla ya vituo vya kuandikisha wapiga kura 406. Kwa siku ya leo siku ya kwanza vituo vimefunguliwa mapema saa 2:00 asubuhi ambapo wananchi wengi wamejitokeza na kutumia haki yao ya msingi ya kujiandikisha na kuboresha taarifa zao
Amesema baada ya vituo kufunguliwa amepita kwenye vituo mbalimbali katika kata za Ndugumbi, Kata ya Magomeni, Kata ya Kinondoni, Kata ya Mwananyamala na Kata ya Kijotonyama na kwamba mwitiko ni mkubwa wananchi wamejitokeza kwa wingi kwa ajili ya kujiandikisha na kuboresha taarifa zao.
“Baada ya kupitia maeneo hayo kuna vituo viwili ambavyo tulibaini vina idadi kubwa ya wananchi hasa Kata ya Ndugumbi Kituo cha Vigaeni ambapo tulielekeza mashine ya BVR moja iongezwe ili iweze kusaidia kupunguza idaidi ya watu ambao wamejitokeza.” Amesema Ndg. Omary na kuongeza’
“Nitoe wito kwa wananchi wote wa Jimbo la Kinondoni na Kawe waweze kutumia fursa hii ya uandikishaji wa wapiga kura ambapo zoezi hili litadumu kwa siku saba. Kwa hiyo wanachi wote tujitokeze kwenye vituo vyetu kwa sababu hali ya vifaa iko vizuri na usalama upo wa kutosha. Kama tunavyofahamu Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura Ni Msingi wa Uchaguzi Bora.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Mkoa wa Dar es Salaam umeanza leo tarehe 17 Machi na kumalizika tarehe 23 Machi, 2025.