Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

INEC yafanya uteuzi wa Madiwani Wanawake wa Viti Maalum

Imewekwa: 09 Sep, 2026
INEC yafanya uteuzi wa Madiwani Wanawake wa Viti Maalum

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imefanya uteuzi wa Madiwani Wanawake 19 wa Viti Maalumu kujaza nafasi wazi zilizojitokeza katika Halmashauri mbalimbali nchini.

​

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na INEC na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Ndg. Kailima R. K leo tarehe 07 Agosti 2026, Tume imefanya uteuzi huo kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 113 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sura ya 343.

​

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tume imefanya uteuzi huo katika kikao chake kilichofanyika Jijini Dar es Salaam kufuatia taarifa iliyowasilishwa Tume na Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhusu uwepo wa nafasi wazi za Madiwani Wanawake wa Vitri Maalum zilizotokana na vifo, kuvuliwa uanachama na kujiuzulu kwenye halmashauri mbalimbali

 

“Taarifa hiyo iliwasilishwa Tume kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sura ya 343.”, imesema taarifa hiyo.

 

​Madiwani walioteuliwa na halmashauri zao kwenye mabano ni Mgeni Yusufu Ramadhani (Manispaa ya Moshi), Felista Andrea Mchopa (Mji wa Newala), Amina Daniel Swai (Wilaya ya Kondoa), Sophia Athmani Nindi (Wilaya ya Namtumbo), Antonia Malulu Mayombo (Wilaya ya Songwe), Krisensia Angolwisye Kapange (Wilaya ya Mbozi), na Getruda Pasta Mwasaka (Wilaya ya Mbozi).

​

Wengine walioteuliwa ni Mwanahamisi Juma Mwagilo (Wilaya ya Pangani), Mwanabakari Mwamsema Kombo (Wilaya ya Muheza), Changwa Adam Mbwana (Wilaya ya Kilindi), Joyce Godfrey Mhando (Wilaya ya Handeni), Rehema Yohana Kimoleta (Wilaya ya Gairo), Elizabeth James Urio (Wilaya ya Mvomero), na Paulina Mosono Siria (Wilaya ya Simanjiro).

 

Aidha Madiwani Wanawake wa Viti Maalum wengine walioteuliwa ni Mastidia Elizeus Tirweshobwa (Wilaya ya Karagwe), Jalunde Massudi Njiwa (Wilaya ya Sikonge), Agripina Mussa Silodi (Wilaya ya Buhigwe), Sylvana Didacus Ndemera (Wilaya ya Rorya), pamoja na Nyamisi Malima Bwire (Wilaya ya Bunda).