Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Mwenyekiti Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi aongoza wajumbe wa tume hiyo kupiga kupiga kura Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Imewekwa: 27 Nov, 2024
Mwenyekiti Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi aongoza wajumbe wa tume hiyo kupiga kupiga kura Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe.Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele,  leo tarehe 27 Novemba 2024 amewaongoza wajumbe wa tume hiyo kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika leo wakiwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Mhe. Jaji Mwambegele amepiga kura katika kituo cha Shule ya Sekondari Jamhuri kililichopo Halmashari ya Jiji la Ilala Mkoani Dar es Salaam akifuatiwa na Mjumbe wa Tume Huru Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari aliyepiga kura katika kituo cha Serikali ya Mtaa Masaki iliyopo Halmashari ya Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam.

Wajumbe wengine waliopiga kura leo ni Mjumbe wa Tume Huru Mhe. Balozi  Omar Ramadhan Mapuri aliyepiga kura katika kituo cha Serikali ya Mtaa Ali Hassan Mwinyi , kilichopo - Mikocheni Halmashari ya Wilaya ya Kinondoni  huku Mjumbe wa Tume Huru Mhe. Magdalena Rwebangira  akipiga kura katika kituo cha KIJICO , kilichopo - Kijitonyama Halmashari ya Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani yeye amepiga kura katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi Chadulu kilichopo Kata ya Makole katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. 

Akizungumza baada ya kupiga kura Mhe. Jaji (Rufaa) Mwambegele amesema ametekeleza jukumu hilo kwa kuwa ni haki yake kupiga kura na kwamba uturatibu uliopo kwenye vituo umewekwa vizuri ili kuwawezesha wapiga kura kutekeleza haki hiyo bila usumbufu.

Mhe. Jaji Mwambegele amewasihi wapiga kura waliojiandikisha kwenda kutekeleza haki yao ya kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka.

Aidha, Bw.Kailima amewaasa wananchi wajitokeze kupiga kura kuwachagua wanyeviti wa serikali ya mtaa, kijiji au kitingoji, wajumbe wanawake na wajumbe mchanganyiko katika maeneo yao. 

Amesema zoezi la kupiga kura halichukui muda mrefu kwani ndani ya dakika mbili unakamilisha haki ya kikatiba kuchagua viongozi katika uchaguzi huo.

Hivyo, amewasihi watanzania wote kwa ujumla na wapiga kura wa mtaa wa Chimuli II kufika kwenye vituo vya kupigia kura na kutekeleza haki yao ya kikatiba.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unafanyika leo nchini baada ya wiki moja ya kampeni za uchaguzi na vituo vya kupigia kura vimefunguliwa saa 2.00 asubuhi na vitafungwa saa 10:00 jioni.