Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Mwenyekiti wa INEC awataka watendaji wa vituo vya kuandikisha wapiga kura Chunya kufanya kazi kwa uaminifu ili kufanikisha uboreshaji wa Daftari

Imewekwa: 24 Dec, 2024
Mwenyekiti wa INEC awataka watendaji wa vituo vya kuandikisha wapiga kura Chunya kufanya kazi kwa uaminifu ili kufanikisha uboreshaji wa Daftari

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (Rufaa) Mhe. Jacobs Mwambegele amewataka washiriki wa mafunzo kwa waandishi wasaidizi na waendesha kifaa cha bayometriki katika Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu ili kufanikisha uboreshaji wa Daftari.

Mhe. Mwambegele ameyasema hayo wakati alipotembelea mafunzo kwa waandishi wasaidizi na waendesha kifaa cha bayometriki yaliyofanyika katika Wilaya ya Chunya Mkoa  wa Mbeya ikiwa ni maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Amesema kuwa kazi ya uboreshaji wa Daftari ni kazi muhimu kwa taifa la Tanzania kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, hivyo amewasihi washiriki hao wazingatie uaminifu katika kutekeleza majukumu yao.

“Kazi ya uboreshaji wa Daftari ambayo mmepangwa kuifanya ni kazi muhimu kwa taifa letu tukielekea kwenye uchaguzi mkuu mwakani. Mimi niwasihi ndugu washiriki kwamba mmeamini kwenda kuitekeleza”, amesema Mhe. Mwambegele na kuongeza kuwa;

“Kwa hiyo katika kuitekeleza kazi hii mnahitajika kuwa waaminifu. Lakini pia lengo la kuwaleta hapa ni kuwafundisha na wengine tunawakumbusha ili kazi hii ikatekelezeke vizuri.

Amewataka washiriki ambao ni wazoefu katika kutekeleza kazi hiyo wawafundishe vizuri ambao si wazoefu ili watakapokwenda kutekeleza jukumu hilo kazi ifanyike vizuri.

Ameongeza kuwa endapo watakutana na changamoto zozote katika utendaji kazi wao wasisite kuwasiliana na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa ufafanuzi au kwa maelekezo mengine yoyote.

Kwa uapnde wake Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Dkt. Zakhia Mohamed Abubakar amewataka washiriki wa mafunzo hayo katika Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya kuhakikisha wanaelewa wanayofundishwa ili waweze kutekeleza jukumu lao kwa weledi na ufasaha.

Amesema waandishi wasaidizi na waendesha kifaa cha bayometriki  ni watendaji  muhimu katika kufanikisha uboreshaji wa Daftari kwa sababu wao ndio wataowaandikisha wapiga kura. Hivyo amewataka waende wakaitekeleza kazi yao kwa ufanisi na ushirikiano.

Kwa upande wa washiriki wa mafunzo hayo wilayani Chunya wameiahidi Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwamba watatekeleza jukumu la uboreshaji wa Daftari kama walivyoelekezwa ili kufanikisha zoezi hilo.

Nasra Hassan Mkupete, mkazi wa Kata ya Mbugani katika Wilaya ya Chunya ameishukuru Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kufanya kazi nzuri ya kuwachagua watu sahihi ambao watakwenda kutekeleza kazi ya uboreshaji wa Daftari kwa ufanisi.

“Kazi ambayo tunakwenda kuzifanya ni uboreshaji wa  Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kwa maana kama mpiga kura amehama kutoka mkoa au kata moja kwenda nyingine, anakwenda kuhamisha taarifa zake” amesema Nasra na kufafanua kuwa:

“Lakini pia tunakwenda kuandikisha wapiga kura wapya ambao hawakuwahi kujiandikisha kwenye Daftari ambao ni wale waliofikisha umri wa  miaka 18.Wale ambao wamepoteza kadi zao za kupigia kura na wale ambao tunakwenda kuwaondoa kwenye Daftari  kutokana na sababu mbalimbali kwa mfano kifo”

“Ninachoahidi kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwamba tutakwenda kufanya kazi kama walivyotuagiza  kuhakikisha kila mtanzania anajiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura”

Nasra ametoa rai kwa wananchi wajitokeze kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwani hiyo ndio haki yao kwa sababu wakishajiandikisha wataweza kipiga kura na kuchagua viongozi bora.

Naye Selemani Mogela ambaye ni Mkazi wa Kata ya Matwiga wilayani Chunya amesema kama walivyofundishwa na wakufunzi wao watawajibika kukamilisha kazi ya ubreshaji wa Daftari ili kikamilisha kazi kama walivyoelekezwa katika mafunzo.

Mkazi  wa Vitimanyango Kata ya Makeko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Janeth Stephen amesema wao wananchi  wameshajiandaa kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwani kupiga kura ni haki yao, hivyo wanaisubiri kwa hamu tarehe 27 Desemba,2024 ili wajitokeze kwa wingi  kwenda kujiandikisha na waweze kupiga kura.

Naye Mwenyekiti wa Mafunzo hato Isakwisa Eliud Kaminyoge ambaye ni mshiriki kutoka Kata ya Mtanila  akiwa ni Mwandishi Msaidizi, ameshukuru waendesha mafunzo kwa kutoa mafunzp kwa weledi na kuwawezesha washiriki kupata mafunzo ili wakayatumie katika kazi ya uboreshaji wa Daftari.

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa ya Mbeya na Iringa na Mkoa wa Dodoma katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa unatarajia kuanza Siku ya Ijumaa tarehe 27 Desemba, 2024 na kumalizika Siku ya Alhamisi tarehe 02 Januari, 2025.