Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Mwenyekiti wa INEC, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele amekabidhi Hati kwa Rais Mteule na Makamu wa Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Imewekwa: 01 Nov, 2025
Mwenyekiti wa INEC, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele amekabidhi Hati kwa Rais Mteule na Makamu wa Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele amewakabidhi Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Emmanuel Nchimbi Hati za Rais Mteule na Makamu wa Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 

Akizungumza katika Hotuba kwenye Hafla ya kutoa Hati ya kuchaguliwa kwa Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika viwanja vya Ofisi za Makao Makuu ya Tume – Njedengwa, Dodoma, Mhe. Mwambegele amesema NAWASALIMU KWA JINA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA!

Waheshimiwa Viongozi na wageni waalikwa,

Mosi, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutuwezesha kukutana hapa katika viwanja vya Ofisi za Makao Makuu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi tukiwa salama, wazima na wenye afya njema.

Pili, kwa niaba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, nawashukuru na kuwapongeza nyote kwa kuhudhuria kwenye hafla hii muhimu kama tulivyowaalika ikiwa ni hatua muhimu katika kukamilisha ratiba ya Uchaguzi wa Rais na Wabunge katika Jamhuri ya Muungano na Madiwani kwa Tanzania Bara kwa Mwaka 2025 kwa ngazi ya Kiti cha Rais na Makamu wa Rais.

Kwa umuhimu wa kipekee, nawashukuru wadau wote wa uchaguzi, hasusan vyama vya siasa, wagombea wa nafasi mbalimbali, wapenzi na wanachama wenu kwa kufanya kampeni za kistaarabu na kudumisha amani na utulivu wakati wote wa kampeni. Hongereni sana.

Waheshimiwa Viongozi na wageni waalikwa,

Kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 74(6)(b) na (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, ikisomwa pamoja na Kifungu cha 10(1)(b) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024, Tume imepewa jukumu la kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais na Wabunge kwa Jamhuri ya Muungano na Madiwani kwa Tanzania Bara.

Kwa kuzingatia masharti rejewa, tarehe 29 Oktoba, 2025 Tume iliendesha na kusimamia uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa mwaka 2025.

Kwa niaba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, natoa shukrani za dhati kwa wananchi, wapiga kura, wagombea na vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki katika uchaguzi huu. Aidha, shukrani za pekee nizitoe kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau wa uchaguzi ambao kwa namna moja au nyingine, wameiwezesha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuratibu, kuendesha, kusimamia na kukamilisha mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa salama na amani.

Waheshimiwa Viongozi na wageni waalikwa,

Ibara ya 41(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inaeleza kwamba, baada ya Bunge kuvunjwa au kukitokea jambo jingine lolote lililotajwa katika ibara rejewa, italazimu kufanyika kwa uchaguzi wa Rais ambapo kila chama cha siasa kinachopenda kushiriki katika uchaguzi wa Rais, kitalazimika kuwasilisha kwa Tume jina la mwanachama wake mmoja kinayetaka agombee katika kuombea uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na jina la mwanachama wake mwingine kinayempendekeza kwa nafasi ya Makamu wa Rais.

Katika ibara ya Ibara ya 41(6) na (7) ya Katiba inafafanua kuwa, Mgombea wa kiti cha Rais atatangazwa kuwa amechaguliwa kuwa Rais iwapo akiwa amepata kura nyingi zaidi kuliko mgombea mwingine yeyote.

Ibara hii inafafanua zaidi kwamba, mgombea wa kiti cha Rais, akitangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuwa amechaguliwa kuwa Rais hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.

Aidha, ibara ya 47(2) inafafanua kwa ufasaha kuwa, Makamu wa Rais atapatikana kwa kuchaguliwa katika uchaguzi utakaomchagua Rais na kwamba, Mgombea wa kiti cha Rais akichaguliwa basi na Makamu wa Rais atakuwa amechaguliwa vilevile.

Waheshimiwa Viongozi na wageni waalikwa,

Katika uchaguzi uliofanyika tarehe 29 Oktoba, 2025, jumla ya Vyama vya Siasa kumi na saba (17) vilisimamisha wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais. Vyama hivyo ni kama ifuatavyo: -

  1. Chama cha Alliance for African Farmers Party (AAFP) – Mgombea wa Kiti cha Rais alikuwa Mheshimiwa Kunje Ngombale Mwiru na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais alikuwa Mheshimiwa Chum Juma Abdalla.
  2. Chama cha African Democratic Alliance Party (ADA – TADEA) - Mgombea wa Kiti cha Rais alikuwa Mheshimiwa Bussungu Georges Gabriel na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais alikuwa Mheshimiwa Makame Ali Issa.
  3. Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) - Mgombea wa Kiti cha Rais alikuwa Mheshimiwa Wilson Elias Mulumbe na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais alikuwa Mheshimiwa Shoka Khamis Juma.
  4. Chama cha Kijamii (CCK) - Mgombea wa Kiti cha Rais alikuwa Mheshimiwa Mwaijojele David Daud na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais alikuwa Mheshimiwa Masoud Ali Abdalla.
  5. Chama cha Mapinduzi (CCM) - Mgombea wa Kiti cha Rais alikuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais alikuwa Mheshimiwa Dkt. Emmanuel John Nchimbi.
  6. Chama cha Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) - Mgombea wa Kiti cha Rais alikuwa Mheshimiwa Mwalim Salum Juma na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais alikuwa Mheshimiwa Devota Mathew Minja.
  7. Chama cha The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi) - Mgombea wa Kiti cha Rais alikuwa Mheshimiwa Gombo Samandito Gombo na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais alikuwa Mheshimiwa Husna Mohamed Abdalla.
  8. Chama cha Democracy Party (DP) - Mgombea wa Kiti cha Rais alikuwa Mheshimiwa Abdul Juma Mluya na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais alikuwa Mheshimiwa Sadoun Abrahman Khatib.
  9. Chama cha MAKINI - Mgombea wa Kiti cha Rais alikuwa Mheshimiwa Coaster Jimmy Kibonde na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais alikuwa Mheshimiwa Azza Haji Suleiman.
  10. Chama cha National Convention for Construction and Reform (NCCR – Mageuzi) - Mgombea wa Kiti cha Rais alikuwa Mheshimiwa Ambar Khamis Haji na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais alikuwa Mheshimiwa Evaline Wilbard Munisi.
  11. Chama cha The National League for Democracy (NLD) - Mgombea wa Kiti cha Rais alikuwa Mheshimiwa Doyo Hassan Doyo na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais alikuwa Mheshimiwa Chausiku Khatib Mohammed.
  12. Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA) - Mgombea wa Kiti cha Rais alikuwa Mheshimiwa Almas Hassan Kisabya na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais alikuwa Mheshimiwa Ali Khamis Hassan.
  13. Chama cha Sauti ya Umma (SAU) - Mgombea wa Kiti cha Rais alikuwa Mheshimiwa Kyara Majalio Paul na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais alikuwa Mheshimiwa Satia Mussa Bebwa.
  14. Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) - Mgombea wa Kiti cha Rais alikuwa Mheshimiwa Rwamugira Mbatina Yustas na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais alikuwa Mheshimiwa Amana Suleiman Mzee.
  15. Chama cha United Democracy Party (UDP) - Mgombea wa Kiti cha Rais alikuwa Mheshimiwa Saum Hussein Rashid na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais alikuwa Mheshimiwa Juma Khamisi Faki.
  16. Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD) -  Mgombea wa Kiti cha Rais alikuwa Mheshimiwa Noty Mwajuma Mirambo na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais alikuwa Mheshimiwa Mashavu Alawi Haji; na
  17. Chama cha United People’s Democracy Party (UPDP) - Mgombea wa Kiti cha Rais alikuwa Mheshimiwa Twalib Ibrahim Kadege na Mgombea nafasi ya Makamu wa Rais alikuwa Mheshimiwa Abdalla Mohamed Khamis.

Waheshimiwa Viongozi na wageni waalikwa,

Leo tarehe 01 Novemba, 2025 kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 41(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 ikisomwa pamoja na kifungu cha 45(9) na (10) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, Tume ilimtangaza mgombea aliyeshinda uchaguzi wa Kiti cha Rais kwa kupata idadi ya kura 31,913,866 sawa na asilimia 97.66 ya kura 32,678,844 halali zilizopigwa. Mgombea aliyetangazwa kuwa mshindi wa Kiti cha Rais ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Emmanuel John Nchimbi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Leo tarehe 01 Novemba, 2025 tuko hapa ili Tume kwa kuzingatia masharti ya kanuni ya 57(5) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025, iweze kumkabidhi hati ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na hati ya kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Emmanuel John Nchimbi.

Baada ya kusema hayo na kwa niaba ya Tume  nawaomba niwakabidhi hati hizo.

Mungu Ibariki Afrika,

Mungu Ibariki Tanzania

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA