Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Mwenyekiti wa INEC Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele atembelelea mafunzo ya siku moja ya Makarani Waongozaji Wapiga Kura katika kata ya Nonde, Jijini Mbeya

Imewekwa: 31 Oct, 2026
Mwenyekiti wa INEC Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele atembelelea mafunzo ya siku moja ya Makarani Waongozaji Wapiga Kura katika kata ya Nonde, Jijini Mbeya

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele leo tarehe 31 Oktoba, 2026 ametembelea mafunzo ya siku moja ya Makarani Waongozaji Wapiga Kura katika kata ya Nonde iliyopo Halmashauri ya Jiji la Mbeya Mkoani Mbeya, yanayofanyika katika ukumbi wa Mkapa ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi Mdogo wa Udiwani wa Kata ya Nonde unaotarajiwa kufanyika tarehe 04 Novemba,2026.

Jaji Mwambegele  amewasisitiza washiriki hao  kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia Sheria na Kanuni ili kuufanya uchaguzi huo kuwa huru na wa haki. 

Awali kabla ya ufunguzi wa Mafunzo haya, washiriki hao waliapa kiapo cha kutunza siri na kile cha kujitoa uanachama wa chama cha siasa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa haki na weledi.

Naye Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Chamwino, Ndugu. Godfrey Mnyamale amefungua Mafunzo kwa Makarani Waongozaji Wapiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Chamwino, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Manchali, Wilayani humo, Mkoa wa Dodoma.

Mbali na Jimbo la Chamwino, uchaguzi mdogo wa madiwani utafanyika katika kata za Lugenge, Halmashauri ya Mji Njombe; Bargish, Halmashauri ya Mji Mbulu; Makole, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na Mwera, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani.

Kata nyingine ni na Oldonyosambu, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Igalula iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Uyui; Shelui, Halmashauri ya Wilaya ya Iramba; Mvumi, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa; Nyarero, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Ilolangulu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe.

.