Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi asema majimbo yanayopendekezwa kuganywa au kubadilishwa majina yatatangazwa kwa kuzingatia Katiba na Sheria

Imewekwa: 26 Apr, 2025
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi asema majimbo yanayopendekezwa kuganywa au kubadilishwa majina yatatangazwa kwa kuzingatia  Katiba na Sheria

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele amesema majimbo yanayopendekezwa kuganywa au kubadilishwa majina yatatangazwa baada ya kikao cha Tume kuchatakata taarifa zote kwa kuzingatia masharti ya Katiba na sheria za Uchaguzi.

Mhe. Jaji Mwambegele ameyasema hayo leo wakati akizungumza kwenye kikao cha pamoja kati ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na wadau wa uchaguzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida mkoani Singida.

Kikao kimefanyika kwa lengo la kuthibitisha maombi yaliyowasilishwa Tume yanayopendekeza kubadilisha jina la Jimbo la Singida Kaskazini, Halmashauri ya Wilaya ya Singida Mkoa wa Singida kwamba ni sahihi kwa mujibu wa barua iliyowasilishwa na Katibu Tawala wa Mkoa.

Mhe. Jaji Mwambegele amewaambia wadau wa uchaguzi kuwa baada ya kufanyika kwa kikao hiko, haina maana kwamba ombi lao limekubaliwa, bali Tume imetimiza matakwa ya kanuni ya 18 ya Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za mwaka 2024 za kutembelea majimbo yaliyoomba kugawanywa au kubadili jina.

“Hivyo, Tume itakutana na kuendelea kuchakata taarifa zote na baada ya hapo kwa kuzingatia masharti ya Katiba na Sheria, itatangaza majimbo yaliyogawanywa na au kubadilisha majina,”alisema Jaji Mwambegele.

Kwa upande wake Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Mahakama Kuu Asina Omari amehudhuria kikao kama hicho kilichofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Mkoa wa Kigoma.

Katika kikao hicho ombi liliwasilishwa Tume kuhusu kupendekeza kubadilisha jina la Jimbo la Buyungu lililopo katika halmashauri hiyo ambapo Tume imethibitisha kuwa ombi hilo ni sahihi kwa mujibu wa barua iliyowasilishwa na Katibu Tawala wa Mkoa.wa Kigoma.

“Aidha naomba kuwasihi tena kwamba kukamilika kwa kikao hiki haina maana kwamba sasa ombi lenu limekubaliwa, bali Tume imetimiza matakwa ya kanuni ya 18 ya Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za mwaka 2024 kwa kutembelea jimbo hilo ambalo limeomba kubadilishwa jina.” amesema Mhe. Jaji Asina.

Ameongeza kuwa Tume itakutana na kuchakata taarifa zote na baada ya hapo kwa kuzingatia masharti ya Katiba na Sheria, itatangaza majimbo yaliyogawanywa na au kubadilisha majina.