Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi atangaza uboreshaji wa Daftari mikoa ya Lindi, Mtwara na wilaya za Madaba, Namtumbo na Tunduru

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mh. Jacobs Mwambegele ametangaza Januari 28,2025 kuanza kwa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa muda wa siku Saba kwa Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma katika halmashauri ya Wilaya za Madaba, Namtumbo na Tunduru.
Jaji Mwambegele amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Tume na Wadau wa Uchaguzi kuhusu Uboreshaji wa Daftari uliofanyika tarehe 16 Januari, 2025 Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Amesema uboreshaji huo utafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 28 Januari, 2025 na kukamilika tarehe 03 Februari mwaka 2025 na vituo vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
Mkoani Lindi, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa Mh. Mbarouk Salim Mbarouk amefungua mkutano kama huo wa wadau wa cuahgzu.
Akifungua mkutano huo Mhe. Jaji Mst. Mbarouk amewatahadharisha wananchi kutojiandikisha zaidi ya mara moja kwenye Daftari la Kudumu la Wapiag Kura kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai.
“Kujiandikisha kuwa mpiga kura zaidi ya mara moja ni kosa la jinai kwa kuzingatia masharti ya kifungua cha 114(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024.” amesema Jaji Mst. Mbarouk na kuongeza:
“Kifungu hicho kinaeleza kuwa yeyote atakayeomba kuandikishwa zaidi ya mara moja kwenye Daftari la Kudumu la Wapiag Kura, atakuwa ametenda kosa la jinai na akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua kiasi cha Sh. 100,000 na isiyozidi Sh. 300,000 au kutumikia kifungo kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili gerezani au vyote kwa pamoja.”
Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi Ndugu Kailima Ramadhani akiwasilisha mada ya uboreshaji wa Daftari mkoani Mtwara, pamoja na mambo mengine amezungumzia umuhimu wa viongozi wa vyama vya siasa kwenye uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Amesema Tume inategemea kuona viongozi wa vyama vya siasa wanawahamasisha wanachama, wafuasi na mashabiki wao kujitokeza kwa siku zote saba badala ya kusema siku saba hazitoshi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura Bi . Giveness Aswile ambaye amewasilisha mada ya Mkurugenzi wa Uchaguzi mkoani Lindi, ameeleza umuhimu wa viongozi wa dini katika uboreshaji wa Daftari.
Amesema viongozi wa dini watakaposimama kwenye madhabahu na mimbari kuwahamasisha wananchi kushiriki zoezi la uboreshaji wa Daftari si dhambi wala halijakatazwa wakitumia fursa na maeneo yao kuwakumbusha watu wao kuhusu tarehe ya zoezi, sifa na wanaohusika kwenye uboreshaji huo.
Mzunguko wa Kumi wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kwa Halmashauri za Wilaya ya Madaba, Namtumbo na Tunduru, unafanyika kuanzia tarehe 28 Januari hadi tarehe 03 Februari, 2025 chini ya Kauilimbiu inayosema ‘Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora’.