Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (Rufaa) Mhe. Jacobs Mwambegele aongoza wajumbe wa Tume kutembelea vituo vya uboreshaji wa Daftari Mkoa wa Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele amewaongoza wajumbe wa Tume kutembelea vituo vya kuandikisha wapiga kura katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ulioanza leo tarehe 17 Machi, 2025 katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mhe. Jaji wa Rufani Mwambegelea ametembelea vituo vya kuandikisha wapiga kura katika Jiji la Dar es Salaam wakati Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk akitembelea vituo vya kuandikisha wapiga kura katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam.
Kwa upande wake Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Mahakama Kuu, Asina Omari ametembelea na kukagua vituo vya kuandikisha wapiga kura katika Jimbo la Mbagala, lililopo Manispaa ya Temeke
Akizungumza baada ya kutembelea vituo hivyo, Mhe. Jaji Asina amewaasa wananchi wajitokeze kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura ili waweze kutumia haki yao ya kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura au kuboresha taarifa zao.
Mhe. Jaji Asina ametembelea vituo vya kuandikisha wapiga kura katika kata nne za Jimbo la Mbagala lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ikiwa ni siku ya kwanza ya uboreshji wa Daftari katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumzia mwitikio wa wananchi, Mhe. Jaji Asina amesema mwitikio ni mzuri wa wananchi ambao wamejitokeza kwenda kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
“Leo ikiwa ni siku ya kwanza ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Mkoa wa Dar es Salaam mpaka sasa tumetembelea kata nne katika Jimbo la Mbagala ambalo lipo katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke”, amesema Mhe. Jaji Asina na kutaja kata hizo:-
“Kata ya Chamazi, Kata ya Charambe, Kata ya Mianzini na Kata ya Mbagala. Mwitikio ni mzuri sana, wananchi wamejitokeza ikiwa ni siku ya kwanza, vituo vyote tumekuta wanachi wengi wamejitokeza na wanahudumiwa. Vifaa vya kutosha vipo kuwahudumia wananchi waliojitokeza vituoni na watendaji wa vituo wanaendelea kuwahudumia wananchi.”
Mhe. Jaji Asina ameongeza kuwa watendaji wa vituo vya kuandikisha wapiga kura wamezingatia utaratibu na maelekezo waliopewa na Tume na kuhakikisha kuwa makundi maalum yanapewa kipaumbele kujiandikisha au kuboresha taarifa zao.
“Katika kupita vituoni pia tumeona waandishi wasaidizi wanatoa huduma kwa kufuata vipaumbele kwa makundi maalum na pale ambapo kunakuwa labda na sintofahamu miongoni mwa wale waliopo vituoni, waandishi wasaidizi wameendelea kutoa elimu kwa wananchi walioko vituoni wakiwafahamisha kwamba kwa mujibu wa taratibu zetu na maelekezo yetu huduma zinatolewa kwa kipaumbele kwenye wale watu ambao ni makundi maalum lakini sehemu nyingi tumekuta utaratibu huu unazingatiwa.
“Kwa hiyo leo ikiwa ni siku ya kwanza mwitikio umekuwa ni mzuri sana tunaendelea kuwaasa wananchi wajitokeze ili waweze kutumia haki yao ya kujiandikisha kwa wale ambao hawajawahi kuandikshwa au kuboresha taarifa zao kwa wale ambao wanahitaji kuboresha taarifa zao.
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Balozi Omar Ramadhan Mapuri ametembelea vituo vya kuandikisha wapiga kura katika Jimbo la Kibamba lililopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.
Baada ya kutembelea vituo, Mhe. Balozi Mapuri ametoa wito kwa wananchi ambao kadi zao za mpiga kura hazijaharibika, hazijapotea, taarifa zao hazijakosewa, hawajahama maeneo yao ya kiuchaguzi kwamba hawana haja ya kwenda kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura.
“Labda nitoe wito kwa wananchi, si lazima kwa mtu ambaye kadi yake ya mpiga kura haina matatizo, hajahama, haijaharibika au haina taarifa zisizokuwa sahihi, hana haja ya kwenda kwenye kituo. Kwenye kituo tunahitaji watu ambao kadi zao zinahitaji marekebisho”, amesema Mhe. Mapuri.
Aidha, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Magdalena Rwebangira ametembelea vituo mbalimbali vya kuandikisha wapiga kura katika Jimbo la Segerea lililopo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kushuhudia uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura likiendelea kwa wananchi kujitokeza kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Mkoa wa Dar es Salaam umeanza leo tarehe 17 Machi na utamalizika tarehe 23 Machi, 2025.