Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Mwambegele awataka wananchi Busega kutumia haki yao kujiandikisha
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa Mhe.Jacobs Mwambegele leo tarehe 24 Agosti, 2024 amepata fursa ya kuzungumza na wananchi wa Kata ya Nyashimo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Busega Mkoa wa Simiyu wakati akiwa njiani kuelekea mkoani Mara.
Mhe. Jaji Mwambegele wakati akipita katika kata hiyo alikutana na maafisa wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wanaotumia Gari la Elimu ya Mpiga Kura kutoa Elimu ya Mpiga Kura kuhusu Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Baada ya kusalimiana na maafisa hao, Mhe. Jaji Mwambegele ya kuzungumza na wakazi wa Kata ya Nyashimo na kuwataka kutumia haki yao ya kikatiba kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wakati utakapofika.
Akizungumza wakati wa kutoa elimu ya mpiga kura, Afisa wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Loshilu Saning’o amewaeleza wakazi hao kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ipo kwenye maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 na maandalizi hayo ni Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Alisema uboreshaji huo unahusu kuwaandikisha wapiga kura wapya ambao wametimiza sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura ambao ni raia wa Tanzania waliotimiza umri wa miaka 18 au zaidi na kutoa fursa kwa wapiga kura waliojiandikisha kubresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kesho tarehe 25 Agosti, 2024 inakutana na wadau wa uchaguzi katika mikoa ya Mara, Simiyu na Manyara ikiwa ni maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Waoiga Kura unaotarajiwa kufanyika katika mikoa hiyo.