Tangazo la maombi ya mpiga kura kupiga kura ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kituo tofauti na kituo alichojiandikisha

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia masharti ya ibara ya 5(3)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na kifungu cha 42(3) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2024 na kanuni ya 48 (1) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025 inawatangazia wapiga kura wote ambao tarehe 29 Oktoba, 2025 ambayo ni siku ya Uchaguzi Mkuu wanatarajia kuwa katika vituo vya kupigia kura tofauti na vituo walivyojiandikisha, kuwa wanaweza kuwasilisha maombi ya kupiga kura ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kituo cha kupigia kura tofauti na vituo walivyojiandikisha.
Zoezi hili litawahusu wapiga kura waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) au Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
1. SABABU ZA KUWASILISHA MAOMBI
Kwa mujibu wa aya ya 2.0 ya Jedwali la Nne la Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025, maombi ya kupiga kura ya Rais katika kituo cha kupigia kura tofauti na kituo alichojiandikisha mpiga kura yanaweza kuwasilishwa kutokana na sababu zifuatazo:
i. Biashara au safari ya muda mrefu katika eneo husika.
ii. Kuwa masomoni au likizo ya masomo.
iii. Kuhamishwa kituo cha kazi.
iv. Kuwa katika matibabu (mpiga kura awe anaweza kufika kwenye kituo cha kupigia kura).
v. Kuhamishwa makazi.
vi. Kuhukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo kisichozidi miezi sita
gerezani au katika chuo cha mafunzo.
vii. Kuhamishwa gereza au chuo cha mafunzo kwa mfungwa au mwanafunzi wa chuo cha mafunzo anayetumikia adhabu ya kifungo kisichozidi miezi sita.
viii. Kumaliza kutumikia kifungo gerezani au katika chuo cha mafunzo.
ix. Sababu nyingine yoyote ambayo Tume itaona inafaa.
2.UTARATIBU WA KUWASILISHA.MAOMBI
Mpiga kura anayekusudia kupiga kura ya Rais katika kituo cha kupigia kura tofauti na kituo alichojiandikisha anaweza kuwasilisha maombi yake kwa njia mojawapo kati ya njia zifuatazo:-
2.1. Kujaza Fomu Na. 29 kwenye ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo analokwenda kupigia kura
Mpiga kura anaweza kuwasilisha maombi ya kupiga kura ya Rais katika kituo tofauti na kituo alichojiandikisha kwa kujaza Fomu Na. 29 ambayo inapatikana katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi katika jimbo la uchaguzi ambalo mpiga kura atakuwepo siku ya kupiga kura tarehe 29 Oktoba, 2025. Baada ya kujaza fomu, mpiga kura ataikabidhi kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo ambalo kuna kituo cha kupigia kura ambacho mpiga kura anakusudia kupigia kura ya Rais siku ya uchaguzi tarehe 29 Oktoba, 2025.
2.2. Kuwasilisha maombi kwa njia ya ki-elektroniki
Mpiga kura anayekusudia kupiga kura kwenye kituo tofauti na alichoandikishwa, anaweza kuwasilisha maombi kwa njia ya kielektroniki kupitia tovuti ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, www.inec.go.tz au moja kwa moja kupitia anuani ya mfumo krp.inec.go.tz ambapo mpiga kura atapatiwa maelekezo ya namna ya kukamilisha maombi yake kabla ya kuyatuma Tume kwa ajili ya uamuzi.
3. MUDA WA KUWASILISHA MAOMBI
Maombi kwa njia ya kujaza fomu Na. 29 kwa msimamizi wa uchaguzi au kwa njia ya ki-elektroniki kupitia tovuti ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, www.inec.go.tz au moja kwa moja kupitia anuani ya mfumo krp.inec.go.tz yanapaswa kuwasilisha ndani ya muda wa siku kumi na nne (14) kuanzia tarehe 19 Septemba, 2025 hadi tarehe 02 Oktoba, 2025 saa 10:00 Alasiri. Aidha, maombi yote yatakayopokelewa baada ya tarehe 02 Oktoba, 2025 hayatafanyiwa kazi.
4. TAARIFA YA KUKUBALIWA AU KUKATALIWA KWA MAOMBІ
Waombaji ambao watakubaliwa kupiga kura ya Rais katika vituo vya kupigia kura tofauti na vituo walivyojiandikisha, watataarifiwa ndani ya siku nane (08) kabla ya siku ya uchaguzi kwa njia zifuatazo: -
i. Ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu ya mkononi.
ii. Kupitia kwa wasimamizi wa uchaguzi.
iii. Njia nyingine yoyote kadri Tume itakavyoona inafaa.
Aidha, wasimamizi wa uchaguzi watabandika orodha ya wapiga kura ambao maombi yao yamekubaliwa ndani ya siku nane (08) kabla ya siku ya uchaguzi katika maeneo yafuatayo: -
i. Vituo vya kupigia kura ambavyo taarifa za wapiga kura
zimehamishiwa.
ii. Vituo vya kupigia kura ambavyo wapiga kura hao walijiandikisha ili kuonesha kuwa wamehamishwa kutoka katika vituo hivyo na kupelekwa kwenye vituo walivyoomba kupigia kura moja ya Rais.
Ifahamike kwamba,
i. Uhamisho wa taarifa za mpiga kura katika utaratibu huu utakuwa ni
kwa madhumuni ya kupiga kura_tarehe 29 Oktoba, 2025 sio uhamisho wa kudumu.
ii. Mpiga kura ambaye taarifa zake zimehamishiwa katika kituo
alichoomba kupiga kura ya Rais pekee HATARUHUSIWA KUPIGA
KURA katika kituo alichokuwa amejiandikisha kwa kuwa jina lake
halitaonekana kwenye kituo alichojiandikisha kwa tarehe 29 Oktoba,
2025.
"Kura Yako Haki Yako Jitokeze Kupiga Kura"
Tangazo hili limetolewa leo taręhe 15 Septemba, 2025 na: -
Kailima, R. K
MKURUGENZI WA UCHAGUZI