Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetoa fomu za uteuzi kwa wanachama 36 kutoka vyama 18 vya siasa nchini kugombea nafasi ya Kiti cha Rais na Makamu wa Rais

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetoa fomu za uteuzi kwa wanachama 36 kutoka vyama 18 vya siasa nchini waliopendekezwa na vyama vyao kugombea nafasi ya Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele ameongoza zoezi hilo mbele ya wajumbe wa Tume na wajumbe wa menejimenti ya Tume, kuanzia siku ya Jumamosi ya tarehe 9 Agosti, 2025 hadi leo tarehe 15 Agosti, 2025.
Akitoa maelezo kabla ya kuwakabidhi fomu za uteuzi, Mhe. Jaji Mwambegele amesema utoaji wa fomu hizo umezingatia masharti ya Ibara ya 39(1)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, ikisomwa pamoja na kifungu cha 34(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 na Kanuni ya 20(1) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025.
Mhe. Jaji Mwambegele amewakabidhi wanachama waliopendekezwa begi maalum lenye nakala 40 za Fomu za Uteuzi wa Wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais – Fomu Na. 8A, nakala nane (8) za Tamko la Mgombea Kuheshimu na Kutekeleza Kanuni za Maadili ya Uchaguzi za Mwaka 2025 - Fomu Na. 10.
Nyaraka nyingine alizowakabidhi ni nakala mbili (2) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, nakala mbili (2) za Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, Nakala mbili (2) za Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024 na nakala mbili (2) za Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025.
Nyingine ni nakala mbili (2) za Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za Mwaka 2024, nakala mbili (2) za Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025 na nakala mbili (2) za Vitabu vya Maelekezo kwa Vyama vya Siasa na Wagombea na walipatiwa barua yenye kuonesha namba ya akaunti kwa ajili ya malipo ya fedha za dhamana.
"Waheshimiwa mliopendekezwa kugombea nafasi ya Kiti cha Rais na Makamu wa Rais, tunawasihi mkazisome nyaraka zote tunazowapatia leo, ili ziweze kuwasaidia katika ujazaji wa fomu za kuomba kuteuliwa kuwa wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais, kufanya kampeni na michakato yote ya uchaguzi.” amesema Mhe. Jaji Mwambegele.
Mbali na kuwasihi kusoma nyaraka hizo, Mhe. Jaji Mwambegele amewatakia kila la kheri wanachama hao waliopendekezwa kugombea nafasi hizo katika kukamilisha kazi kubwa iliyo mbele yao.
Wanachama waliopatiwa fomu za uteuzi ni Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kugombea nafasi ya Kiti cha Rais na Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Hassan Kisabya Almas (Kiti cha Rais) na Mhe. Hamisi Ally Hassan (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA).
Wengine ni Mhe. Kunje Ngombale Mwiru (Kiti cha Rais) na Mhe. Shum Juma Abdalla (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Alliance for African Farmers Party (AAFP), Mhe. Doyo Hassan Doyo (Kiti cha Rais) na Mhe. Chausiku Khatib Mohamed (Kiti cha Makamu wa Rais) wa Chama cha National League for Democracy (NLD) na Mhe. Coster Jimmy Kibonde (Kiti cha Rais) na Mhe. Aziza Haji Suleiman (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Makini (MAKINI).
Wanachama wengine ni Mhe. Twalib Ibrahim Kadege (Kiti cha Rais) na Mhe. Abdalla Mohd Khamisi (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha United People's Democratic Party (UPDP), Mhe. Georges Gabriel Bussungu (Kiti cha Rais) na Mhe. Ali Makame Issa (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Tanzania Democratic Alliance (TADEA), na Mhe. Mwajuma Noty Mirambo (Kiti cha Rais) na Mhe. Mashavu Alawi Haji (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD),
Mhe. Yustas Mbatina Rwamugira (Kiti cha Rais) na Mhe. Amana Suleiman Mzee (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Mhe. David Daud Mwaijojele (Kiti cha Rais) na Mhe. Masoud Ali Abdala (Kiti cha Makamu wa Rais) wa Chama cha Kijamii (CCK), Mhe. Salum Mwalimu (Kiti cha Rais), Mhe. Devotha Mathew Minja (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).
Wengine ni Mhe. Abdul Juma Mluya (Kiti cha Rais) na Mhe. Sadoun Abrahman Khatib (Kiti cha Makamu wa Rais) wa Chama cha Democratic Party (DP) na Mhe. Majalio Paul Kyara (Kiti cha Rais) na Mhe. Satia Mussa Bebwa (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU).
Aidha, wanachama wengine ni Mhe. Gombo Samandito Gombo (Kiti cha Rais) na Mhe. Husna Mohamed Abdalla (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Mhe. Wilson Elias Mulumbe (Kiti cha Rais) na Mhe. Shoka Khamis Juma wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC).
Siku ya mwisho ya utoaji fomu za uteuzi imekamilika kwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele kutoa fomu kwa Mhe. Saum Hussein Rashid (Kiti cha Rais) na Mhe. Juma Khamis Faki wa Chama cha United Democratic Party (UDP), Mhe. Haji Ambar Khamis (Kiti cha Rais) na Mhe. Dkt. Eveline Wilbard Munisi (Kiti cha Makamu wa Rais) wa Chama cha National Convention for Construction and Reform – Mageuzi (NCCR-MAGEUZI), Mhe. Luhaga Joelson Mpina (Kiti cha Rais) na Mhe. Fatma Abdulhabib Ferej (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT - WAZALENDO).
Baada ya kukamilika kwa utoaji wa fomu za uteuzi kwa wananchama waliopendekezwa kugombea nafasi ya kiti cha Rais na Makamu wa Rais, kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi iliyotangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, wanachama hao wanapaswa kujaza fomu hizo na kuzirejesha ifikapo siku ya uteuzi wa wagombea ambayo ni tarehe 27 Agosti, 2025.
Ikumbukwe kuwa, wakati utoaji wa fomu za uteuzi kwa nafasi ya Kiti cha Rais na Makamu wa Rais ukikamilika, utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea kwa nafasi ya Ubunge kwa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania na Madiwani kwa Tanzania Bara, umeanza tarehe 14 Agosti, 2025 na utakamilika tarehe 27 Agosti, 2025 ambayo itakuwa siku ya uteuzi wa wagombea.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo iliyotangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, kampeni za uchaguzi zinatarajia kuanza tarehe 28 Agosti, 2025 hadi tarehe 28 Oktoba, 2025 kwa Tanzania Bara wakati kipindi cha kampeni za Uchaguzi kwa Tanzania Zanzibar itakuwa tarehe 28 Agosti, 2025 hadi 27 Oktoba, 2025 ili kupisha kura ya mapema na Tarehe 29 Oktoba, 2025 siku ya Jumatano itakuwa ndiyo Siku ya Kupiga Kura.