Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka watendaji wa uchaguzi kutoa ajira za watendaji wa vituo kwa watu wenye sifa na uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka watendaji wa uchaguzi kutoa ajira za watendaji wa vituo kwa watu wenye sifa na uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi.
Rai hiyo imetolewa na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama Kuu Asina A. Omari, wakati akifungua mafunzo kwa Watendaji wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo kwa mikoa ya Mwanza na Mara ambapo amewasisitiza kuwa wasitoe ajira hizo kwa kuwapendelea ndugu na jamaa zao ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi.
"Ajira za Watendaji wa vituo zizingatie kuajiri Watendaji wenye weledi, wanaojitambua, wazalendo, waadilifu na wachapakazi na kuachana na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi" Ameeleza Jaji Asina.
Aidha, Mhe. Jaji Asina amewataka Watendaji hao kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili waweze kubaini mahitaji maalum ya vituo husika na kuhakikisha kunakuwa mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.
Mafunzo hayo ambayo yanatarajiwa kukamilika Julai 23, 2025, ni sehemu ya kuwajengea uwezo watendaji hao kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.