Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewateua Mhe. Luhaga Joelson Mpina kuwa Mgombea wa Kiti cha Rais na Mhe. Fatma Abdulhabib Ferej kuwa Mgombea wa Kiti cha Makamu wa Rais kupitia ACT - WAZALENDO

Imewekwa: 13 Sep, 2025
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewateua Mhe. Luhaga Joelson Mpina kuwa Mgombea wa Kiti cha Rais na Mhe. Fatma Abdulhabib Ferej kuwa Mgombea wa Kiti cha Makamu wa Rais kupitia ACT - WAZALENDO

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewateua Mhe. Luhaga Joelson Mpina kuwa Mgombea wa Kiti cha Rais na Mhe. Fatma Abdulhabib Ferej kuwa Mgombea wa Kiti cha Makamu wa Rais kupitia Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT - WAZALENDO).

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele amefanya uteuzi huo leo tarehe 13 Septemba, 2025 kutokana na Shauri la Kikatiba Na. 21692 la Mwaka 2025 lililofunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu Dodoma kwa hati ya dharura tarehe 27 Agosti, 2025.

Shauri hilo lilifunguliwa na Bodi ya Wadhamini ya Chama cha ACT- Wazalendo na Luhaga Joelson Mpina dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kupinga uamuzi wa Tume kumzuia Ndugu Luhaga Joelson Mpina kurejesha fomu ya uteuzi tarehe 27 Agosti, 2025.

Mhe. Jaji Mwambegele amefanya uteuzi huo kutimiza masharti ya Ibara ya 39(1), 41 na 47(4) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, zikisomwa pamoja na kifungu cha 34 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 na kwa mujibu wa kanuni ya 20(5) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025.

Baada ya uteuzi huo, Mhe. Jaji Mwambegele amewakabidhi wagombea hao seti moja ya fomu za uteuzi pamoja na nakala moja ya Tamko la Kuheshimu na Kutekeleza Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025 kwa ajili ya kumbukumbu zao.

Uteuzi huo wa wagombea kupitia ACT-Wazalendo umetimiza idadi ya wagombea 36 wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais kutoka vyama 18 vya siasa vilivyochukua fomu za uteuzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 uliopangwa kufanyika siku ya Jumatano tarehe 29 Oktoba, 2025.

Mhe. Jaji Mwambegele amemkabidhi Mhe. Luhaga Joelson Mpina gari moja jipya aina ya Landcruiser GX VXR pamoja na dereva kwa ajili ya kampeni za uchaguzi.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa ACT- Wazalendo Ndg. Omar Issa Shaaban ameishukuru Tume kwa kutoa gari hilo na kueleza uamuzi wa chama hicho kuiomba Tume kulitumia gari hilo kwa matumizi mengine kwani chama kinalo gari kwa ajili ya kampeni isipokuwa watahitaji mlinzi kwa ajili ya mgombea wa kiti cha Rais.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele amekubaliana na uamuzi huo wa ACT-Wazalendo kwa kuwa lengo la Tume ni kuweka uwanja sawa wa kampeni na kuwatakia mafanikio katika kampeni.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Ndg. Kailima Ramadhani ameongoza zoezi la kubandika fomu za uteuzi za wagombea hao nje ya ofisi ndogo ya Tume iliyopo Jijini Dar es Salaam ili kutoa fursa ya kuweka pingamizi dhidi ya uteuzi wa wagombea husika.

Pingamizi hilo linaweza kuwekwa na mgombea mwingine, Msajili wa Vyma vya Siasa au Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanzia leo tarehe 13 Septemba 2025, Saa 10:00 Jioni, hadi kesho tarehe 14 Septemba, 2025 Saa 10:00 Jioni.   

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 zinaendelea hadi tarehe 28 Oktoba, 2025 kwa Tanzania Bara na tarehe 27 Oktoba, 2025 kwa Tanzania Zanzibar ili kupisha kura ya mapema.

Kura Yako Haki Yako Jitokeze Kupiga Kura