Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi yafanya uteuzi wa wagombea 34 wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais

Imewekwa: 27 Aug, 2025
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi yafanya uteuzi wa wagombea 34 wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imefanya uteuzi wa wagombea 34 wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais kutoka vyama 17 vya siasa vilivyochukua fomu za uteuzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 uliopangwa kufanyika siku ya Jumatano tarehe 29 Oktoba, 2025.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele amefanya uteuzi huo baada ya wanachama waliopendekezwa kutimiza masharti ya Ibara ya 39(1), 41 na 47(4) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, zikisomwa pamoja na kifungu cha 34 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024.

Mhe. Jaji Mwambegele amesema kutokana na kutimiza masharti hayo, kwa mujibu wa kanuni ya 20(5) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewateua wagombea hao.

Baada ya uteuzi huo, Mhe. Jaji Mwambegele amewakabidhi wagombea hao seti moja ya fomu za uteuzi pamoja na nakala moja ya Tamko la Kuheshimu na Kutekeleza Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025 kwa ajili ya kumbukumbu zao.

 

Wagombea walioteuliwa ni Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nafasi ya Kiti cha Rais na Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Hassan Kisabya Almas (Kiti cha Rais) na Mhe.  Hamisi Ally Hassan (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA).

Wengine ni Mhe. Coster Jimmy Kibonde (Kiti cha Rais) na Mhe.  Aziza Haji Suleiman (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Makini (MAKINI), Mhe. Gombo Samandito Gombo (Kiti cha Rais) na Mhe. Husna Mohamed Abdalla (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Mhe. Abdul Juma Mluya (Kiti cha Rais) na Mhe. Sadoun Abrahman Khatib (Kiti cha Makamu wa Rais) wa Chama cha Democratic Party (DP) na Mhe. Kunje Ngombale Mwiru (Kiti cha Rais) na Mhe. Shum Juma Abdalla (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Alliance for African Farmers Party (AAFP).

Walioteuliwa wengine ni Mhe. Saum Hussein Rashid (Kiti cha Rais) na Mhe. Juma Khamis Faki (Makamu wa Rais) wa Chama cha United Democratic Party (UDP), Mhe. Mwajuma Noty Mirambo (Kiti cha Rais) na  Mhe.  Mashavu Alawi Haji (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD) na Mhe. Georges Gabriel Bussungu (Kiti cha Rais) na Mhe.  Ali Makame Issa (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Tanzania Democratic Alliance (ADA-TADEA).

Wengine ni Mhe. Twalib Ibrahim Kadege (Kiti cha Rais) na Mhe. Abdalla Mohd Khamisi (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha United People's Democratic Party (UPDP), na Mhe. Doyo Hassan Doyo (Kiti cha Rais) na Mhe. Chausiku Khatib Mohamed (Kiti cha Makamu wa Rais) wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Mhe. Majalio Paul Kyara (Kiti cha Rais) na Mhe. Satia Mussa Bebwa (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Mhe. Wilson Elias Mulumbe (Kiti cha Rais) na Mhe. Shoka Khamis Juma wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC),

Wanachama wengine walioteuliwa ni Mhe. Haji Ambar Khamis (Kiti cha Rais) na Mhe. Dkt. Eveline Wilbard Munisi (Kiti cha Makamu wa Rais) wa Chama cha National Convention for Construction and Reform – Mageuzi (NCCR-MAGEUZI), Mhe. David Daud Mwaijojele (Kiti cha Rais) na Mhe.  Masoud Ali Abdala (Kiti cha Makamu wa Rais) wa Chama cha Kijamii (CCK), Mhe. Salum Mwalimu (Kiti cha Rais), Mhe. Devotha Mathew Minja (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), na Mhe. Yustas Mbatina Rwamugira (Kiti cha Rais) na Mhe.  Amana Suleiman Mzee (Kiti cha Makamu wa Rais) kupitia Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), 

Mhe. Jaji Mwambegele amewapongeza wagombea hao kwa kuteuliwa na kuwatakia kampeni zenye mafanikio na kuwakabidhi wagombea wa Kiti cha Rais gari moja jipya aina ya Landcruiser GX VXR pamoja na dereva kwa ajili ya kampeni za uchaguzi.

Mbali na uteuzi wa wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais, uteuzi wa wanachama waliochukua fomu za uteuzi kugombea nafasi ya Ubunge kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani kwa Tanzania Bara, umefanyika leo tarehe 27 Agosti, 2025.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo iliyotangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, kampeni za uchaguzi zinatarajia kuanza kesho tarehe 28 Agosti, 2025 hadi tarehe 28 Oktoba, 2025 kwa Tanzania Bara wakati kipindi cha kampeni za Uchaguzi kwa Tanzania Zanzibar itakuwa tarehe 28 Agosti, 2025 hadi 27 Oktoba, 2025 ili kupisha kura ya mapema na Tarehe 29 Oktoba, 2025 siku ya Jumatano itakuwa ndiyo Siku ya Kupiga Kura.

Kura Yako Haki Yako Jitokeze Kupiga Kura