Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi yatangaza kuongeza siku mbili za uboreshaji wa Daftari katika Mkoa wa Dar es Salaam hadi tarehe 25 Machi, 2025

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza kuongeza siku mbili za uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Mkoani Dar es Salaam hadi siku ya Jumanne ya tarehe 25 Machi, 2025.
Hatua hiyo imetangazwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, kufuatia mwitikio mkubwa wa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam ambapo leo tarehe 23 Machi, 2025 ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya uboreshajiwa Daftari ulioatangazwa na Tume awali.
“Hivyo basi, napenda kuwatangazia wananchi wote wa mkoa wa Dar es Salaam kuwa, Tume imeongeza siku mbili za uboreshaji wa Daftari kwa tarehe 24 na 25 Machi, 2025 na zoezi litakamilika tarehe 25 Machi, 2025 saa 12:00 jioni,” amesema Mhe. Jaji Mwambegele.
Jaji Mwambegele amefafanua kuwa Tume haitaongeza siku nyingine baada ya kukamilika kwa siku hizo mbili za nyongeza.
Amesema wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wamekuwa na mwitikio mkubwa katika kujiandikisha na kuboresha taarifa zao tangu siku ya kwanza ya uboreshaji wa Daftari tarehe 17 Machi, 2025 na kuilazimu Tume kuongeza mashine za BVR na watendaji wa vituo vya kuandikisha wapiga kura.
“Kutokana na mwitikio mkubwa Tume ilichukua hatua za kuongeza mashine za BVR kits pamoja na watumishi katika maeneo yote yaliyoonekana kuwa na watu wengi na hatua hii imewezesha zoezi kuendelea kwa utulivu katika maeneo yote,” amesema Mhe. Jaji Mwambegele.
Amesema uamuzi wa Tume wa kuongeza mashina na waendaji wa vituo uliongeza kasi ya kuwahudumia wananchi na kupunguza kwa kiasi kikubwa misongamano ya wananchi kwenye baadhi ya maeneo.
Kutokana na mwitikio huo, Mhe. Jaji Mwambegele amewapongeza wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa mara ya kwanza, kuboresha au kuhamisha taarifa zao na kupata kadi mpya kwa wale ambao kadi zao zimepotea au zimeharibika.
Katika hatua nyingine Jaji Mwambegele ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwa zoezi hilo halihusishi ubadilishaji wa kadi zilizotolewa na Tume tangu 2015 na mwaka 2020.
“Napenda kuwakumbusha kuwa zoezi hili halihusishi ubadilishaji wa kadi za mpiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 kwa kuwa kadi hizo ni halali na zitaendelea kutumika kwa mujibu wa kifungu cha 168 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani,” alisema Jaji Mwambegele na kuongeza;
“Hivyo, wananchi wote ambao kadi zao hazijaharibika au kupotea, hawajahama kutoka kata au halmashauri hawahusiki na zoezi hili”.
Mhe. Jaji Mwambegele amewaonya baadhi ya wananchi wanaojiandikisha zaidi ya mara moja kwa kuwa ni kosa kisheria na anayefanya hivyo akitiwa hatiani anaweza kufungwa jela, kutozwa faini au vyote kwa pamoja.
Amesema kujiandikisha zaidi ya mara moja ni kosa kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 114(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya Mwaka 2024.
“Mtu yeyote akithibitika amejiandikisha zaidi ya mara moja atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua kiasi cha shilingi laki moja (100,000/=) na isiyozidi shilingi laki tatu (300,000/=) au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili gerezani au vyote kwa pamoja, kulipa faini na kifungo gerezani,” amesema Mhe. Jaji Mwambegele.
Ametoa wito kwa wadau wote wa uchaguzi na wananchi kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa Tume na kuhakikisha kuwa wanaokwenda kujiandikisha na kuboresha taarifa zao vituoni ni wale tu ambao wanastahili kufanya hivyo.
Tume imekamilisha mizunguko 12 ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa 30 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tangu ilipozindua uboreshaji wa Daftari katika Mkoa wa Kigoma tarehe 20 Julai, 2024, ambapo Dar es Salaam utakua mkoa wa 31 katika mzunguko wa 13.