Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi yawataka wananchi wa Dar es Salaam waliojiandikisha kwenye Daftari mwaka 2015 na 2020, kadi zao hazijapotea, hazijaharibika au hawajahama wasiende kwenye vituo

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewakumbusha wananchi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwaka 2015 na 2020 na kadi zao za mpiga kura hazijapotea, hazijaharibika au hawajahama maeneo yao walikojiandikisha awali wasiende kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura.
Aidha Tume imewataka wananchi wa Dar es Salaam wenye sifa za kujiandikisha kuwa wapiga kura, wajitokeze kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura vilivyoko katika maeneo.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Tume leo tarehe 19 Machi, 2025 na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Ndg Kailima, R. K, uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unahusisha kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania waliotimiza umria wa miaka 18 na zaidi na hawakuwahi kuandikishwa hapo awali.
Tangazo hilo limetaja mambo mengine yanayohusika kwenye uboreshaji wa Daftari kuwa ni kuandikisha wapiga kura ambao watakuwa wametimiza umri wa miaka 18 siku ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Mambo mengine ni kuboresha taarifa za wapiga kura waliohama kutoka eneo moja kwenda eneo lingine la kiuchaguzi, kutoa kadi mpya kwa wapiga kura ambao kadi zao zimepotea au kuharibika na kuboresha au kurekebisha taarifa za wapiga kura.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, mpiga kura anaweza pia kuwasiliana na Maafisa wa Tume waliopo katika Kituo cha Huduma kwa Mpiga Kura kwa kupiga simu bure kwenda namba 0800112100.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Mkoa wa Dar es Salaam umeanza siku ya Jumatatu ya tarehe 17 Machi, 2025 na utakumalizika tarehe 23 Machi, 2025.