Tume kuwaandikisha wafungwa na wanafunzi wa vyuo vya mafunzo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa mara ya kwanza itawaandikisha wafungwa kwa upande wa Tanzania Bara na wanafunzi wa vyuo vya mafunzo kwa upande wa Zanzibar na kuwaruhusu wapiga kura kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zao kwa njia ya mtandao.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima R. K wakati akifanya mahojiano maalum kwenye kipindi cha Jambo kinachorushwa hewani na kituo cha televisheni cha TBC1 jijini Dar es Salaam leo tarehe 17 Mei, 2024.
Amesema Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaotarajiwa kuanza tarehe 1 Julai, 2024 utakuwa na mambo mapya kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwaandikisha wafungwa.
Ameongeza kuwa mbali na kuwaandikisha wafungwa uboreshaji huo utawaruhusu wapiga kura kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zao kwa njia ya mtandao.
Kailima amefafanua kuwa utaratibu wa kuandikisha wafungwa na wanafunzi utazingatia matwaka ya sheria ambapo waliohukumiwa kifungo cha chini ya miezi sita ndio watakaoandikishwa.
Akizungumzia suala la kuanzisha mchakato wa uboreshaji wa Daftari mtandaoni, Bw. Kailima amesema Tume imejenga mfumo ujulikanao kama OVRS (Online Voters Registration System) utakaomwezesha mpiga kura anayeboresha taarifa zake kuanzisha mchakato mtandaoni na baadae kwenda kwenye kituo ili kukamilisha taratibu na kupata kadi yake ya mpiga kura.
“Uboreshaji wa taarifa kwa njia ya mtandao una masharti, kwa wale ambao wanataka kurekebisha taarifa zao ni lazima wawe na namba ya NIDA, lakini, mpiga kura anayehamisha taarifa zake hatalazimika kuwa na namba ya NIDA….,” amesema Bw. Kailima.
Amefafanua kuwa namba ya NIDA ni muhimu kwa ajili ya kufanya uhakiki wa taarifa za mpiga kura ambazo zinarekebishwa kwenye Daftari.
Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi amefafanua kuwa, wanaokwenda vituoni kujiandikisha kwa mara ya kwanza hawatalazimika kuwa na namba ya NIDA.
Akitoa taarifa ya kutangaza tarehe ya uzinduzi wa uboreshaji wa Daftari ambao unatarajiwa kufanyika mkoani Kigoma tarehe 01 Julai, 2024, Mwemyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele alisema kuwa kwa Tanzania Bara kuna vituo vya kuandikisha wapiga kura 130 vilivyopo kwenye magareza na kwa Zanzibar kuna vituo 10 vilivyopo kwenye Vyuo vya Mafunzo.