Tume yamtangaza Bw.Khamis Yussuf Mussa kuwa mshindi wa Kiti cha Ubunge katika Jimbo la Kwahani
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kupitia Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kwahani-Zanzibar Bi.Safia Iddi Muhammad imemtangaza Bw.Khamis Yussuf Mussa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mshindi wa Kiti cha Ubunge katika Jimbo la Kwahani.
Mussa almaarufu Pele ameibuka mshindi wa kiti hicho baada ya kupata Kura 7,092 Kati ya Kura halali 7,383 zilizopigwa na kuwabwaga wagombea wenzake 13 waliokuwa wakichuana katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo uliofanyika leo tarehe 8 Juni, 2024.
Jimbo la Kwahani lilikuwa na wapiga kura 11,936 na waliojitokeza kupiga kura ni 7,522 ambapo kura 139 zilikataliwa hivyo kufanya kura halali zilizopigwa kuwa ni 7,383.
Vyama 14 vilisimamisha wagombea katika Uchaguzi huo mdogo wa kiti cha Ubunge jimbo la Kwahani lililopo Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi.
Wagombea wengine na kura walizopata katika mabano ni pamoja na Bi. Jarade Ased Khamis wa AAFP (06), Bi. Madina Mwalim Hamad wa ADA TADEA (49), Bi. Shara Amran Khamis wa ADC (83), Bi. Zainab Maulid Abdallah wa CCK (21), Bw. Abdi Khamis Ramadhan wa CUF(79), Bw. Bashir Yatabu Said wa Demokrasia Makaini (14) na Bi. Nuru Abdulla Shamte wa DP(07) .
Wengine ni Bw. Kombo Ali Juma wa NRA (05), Bi. Mwanakombo Hamad Hassan wa NLD (08), Bw. Amour Haji Ali wa SAU(07), Bi. Naima Salum Hamad wa UDP(01), Bi. Mashavu Alawi Haji wa UMD(05) na Bi. Tatu Omary Mungi wa UPDP(06).
Uchaguzi katika Jimbo la Kwahani umefanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ahmed Yahya Abdulwakil (65) kufariki dunia mwezi Aprili mwaka huu.