Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Tume yasema wote wenye sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wataandikishwa hata kama hawana kitambulisho cha NIDA

Imewekwa: 15 Jun, 2024
Tume yasema wote wenye sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wataandikishwa hata kama hawana kitambulisho cha NIDA

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema watu wote wenye sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wataandikishwa hata kama hawana kitambulisho cha Taifa kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bi. Giveness Aswile tarehe 15 Juni, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha mada kwenye mkutano wa Tume na Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri.

Mkutano huo unahitimisha mfululizo wa mikutano ambayo Tume imefanya na wadau wake kauanzia tarehe 07 Juni, 2024. Baadae Tume itafanya mikutano na wadau kwenye mikoa yote kwa kuzingatia ratiba ya uboreshaji wa Daftari. 

Mikutano hiyo ina lengo Ia kuwapa wadau taarifa za uwepo wa zoezi la uboreshaji wa Daftari Ia Kudumu la Wapiga Kura na kuwapitisha katika vifaa na mifumo ya uandikishaji pamoja na kuona namna zoezi litakavyofanyika vituoni. 

"Kuwa na kadi ya NIDA sio kigezo cha kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu Ia Wapiga Kura. Wananchi wote wenye sifa wataandikishwa bila kujali kama wana kadi ya NIDA au la," amesema Bi. Aswile. 

Ameyataja mambo yatakayohusika kwenye uboreshaji wa daftari kuwa ni pamoja na kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu 2025 na kutoa fursa kwa wapiga kura waliopo kwenye daftari na ambao wamehama, waweze kuhamisha taarifa zao kutoka kata au jimbo walioandikishwa awali. 

Mambo mengine ni kutoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao yakiwemo majina na taarifa nyingine, kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuukana uraia wa Tanzania au kifo.