Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Tume yatoa vibali kwa asasi 157 kutoa elimu ya mpiga kura na uangalizi kwa asasi 34 wakati wa uboreshaji wa Daftari Mwaka 2024/2025

Imewekwa: 25 Jun, 2024
Tume yatoa vibali kwa asasi 157 kutoa elimu ya mpiga kura na uangalizi kwa asasi 34 wakati wa uboreshaji wa Daftari Mwaka 2024/2025

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetoa vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa asasi za kiraia 157  na kibali cha uangalizi wa uboreshaji kwa asasi 34 za ndani ya nchi.

Vibali hivyo vimetolewa na Tume katika kikao chake cha tarehe 22 na 24 Juni, 2024 kwa kuzingatia kifungu cha 10(1) (g) na (h) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024, ikisomwa pamoja na kanuni ya 46(4) ya kanuni za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura za Mwaka 2024.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Tume leo tarehe 25 Juni, 2024 na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima, R. K, asasi zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura zitajulishwa kwa njia ya barua pepe kupitia Mfumo wa Usajili (Accreditation Management System) ili kujaza taarifa za kuwawezesha kukamilisha taratibu zingine ikiwemo kutaja maeneo ambayo watatoa elimu hiyo na orodha ya watu watakaotoa elimu ya mpiga kura katika maeneo hayo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, majina ya taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura na uangalizi wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura 2024/2025 yatatangazwa kupitia tovuti ya Tume ya www.inec.go.tz na mitandao ya kijamii.

Kufuatia utoaji huo wa vibali, Tume imezipongeza taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura na kuwa waangalizi wa uandikishaji kwa mwaka 2024/2025.

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unatarajiwa kuzinduliwa tarehe 20 Julai, 2024  mkoani Kigoma na Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb).