Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Tume yatoa vibali kwa asasi 4 za kiraia kuangalia na kutoa Elimu ya Mpiga Kura Uchaguzi Mdogo Jimbo la Kwahani, Zanzibar

Imewekwa: 11 May, 2024
Tume yatoa vibali kwa asasi 4 za kiraia kuangalia na kutoa Elimu ya Mpiga Kura Uchaguzi Mdogo Jimbo la Kwahani, Zanzibar

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetoa vibali (kwa asasi nne za kiraia) vya uangalizi na utoaji wa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Kwahani, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.

Kwa kujibu wa taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima, R. K, Tume imefanya uamuzi huo kupitia kikao chake kilichofanyika leo Mjini Unguja, Zanzibar.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Tume imefikia uamuzi huo kwa kuzingatia kifungu cha 85(4) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 na kifungu cha 10(1)(g) na (h) vya Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024.

Vifungu hivyo vinaipa Tume jukumu la kualika waangalizi wa uchaguzi, kutoa elimu ya mpiga kura nchini, kuratibu na kusimamia taasisi na asasi za kiraia zinazotoa elimu hiyo.

Asasi za kiraia zilizopata kibali cha uangalizi katika uchaguzi mdogo wa Ubunge katika jimbo la Kwahani, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, ni Zanzibar Fighting Against Youth Challenges Organization na Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar.

Asasi zilizopata kibali cha kutoa Elimu ya Mpiga Kura ni Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria Wanawake (ZAWOPA) na Shirika la Elimu ya Uraia na Uzalendo Tanzania “Civic Education and Patriotism Association.

“Aidha, katika utekelezaji wa majukumu yao, asasi hizo zitapaswa kuzingatia Mwongozo wa Watazamaji wa Mwaka 2020 na Mwongozo wa Elimu ya Mpiga Kura wa Mwaka 2020 katika kipindi chote cha uchaguzi huu mdogo”, ilisema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:

“Tume inatumia fursa hii kuzipongeza asasi zote za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura na uangalizi. Vile vile, Tume inazikumbusha asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura kuzingatia ratiba ya utoaji wa elimu ya mpiga kura iliyotolewa na Tume.”

Ilifafanua taarifa hiyo kuwa asasi zilizopewa vibali zinapaswa kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo ya Tume katika kipindi chote cha uchaguzi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kibali cha uangalizi kitatumika kipindi chote cha uchaguzi huu mdogo na kibali cha kutoa elimu kitatumika kuanzia tarehe 24 Mei, 2024 hadi tarehe 07 Juni, 2024.

Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Kwahani, Zanzibar utafanyika siku ya Jumamosi tarehe 8 Juni, 2024.