Tume yazialika taasisi na asasi za ndani ya nchi kuangalia uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utakaoanza tarehe 1 Julai, 2024

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetoa mwaliko kwa taasisi na asasi mbalimbali nchini zinazohitaji kuangalia zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kuwasilisha maombi ya kuangalia uboreshaji huo unaotarajiwa kuanza tarehe 1 Julai, 2024.
Mwaliko huo umetolewa kupitia tangazo la leo tarehe 17 Mei, 20224 lililosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Kailima, R. K kwa mujibu wa kanuni ya 46(1) ya Kanuni za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura za Mwaka 2024 kwa kuzingatia ratiba itakayotolewa na Tume.
Kwa mujibu wa tangazo la mwaliko huo taasisi au asasi inayotaka kuangalia uboreshaji huo inatakiwa kupitia anuani (link) ifuatayo: https://ams.inec.go.tz
Barua ya maombi itatakiwa kuainisha mambo yafuatayo: -
- anuani kamili ya taasisi au asasi husika;
- mahali ambapo taasisi au asasi husika inafanyia kazi (Physical address);
- shughuli ambazo zinafanywa na taasisi au asasi husika kwa mujibu wa hati ya usajili;
- sehemu ambazo taasisi au asasi inaomba kwenda kuangalia uandikishaji;
- idadi ya watu ambao taasisi au asasi itawatumia katika zoezi hilo pamoja na majina na taarifa zao binafsi;
- majina na namba za simu za viongozi watatu wa taasisi au asasi;
- ikiwa taasisi au asasi ya ndani inahusisha viongozi ambao si raia wa Tanzania, viongozi wawili ni lazima wawe watanzania;
- kuambatisha nakala au kivuli cha hati ya usajili wa taasisi au asasi husika; na
- kuambatisha nakala au kivuli cha katiba ya taasisi au asasi husika.
Maombi yatakayozingatiwa ni yale yatakayowasilishwa kupitia anuani (link) ifuatayo: https://ams.inec.go.tz
Mwisho wa kupokea maombi ni tarehe 30 Mei, 2024.
Tume haitahusika na utoaji wa rasilimali fedha au rasilimali nyingine kwa ajili ya kugharamia zoezi la uangalizi kwa taasisi au asasi zitakazopewa kibali.