Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Tume yazialika taasisi na asasi za kiraia kutoa Elimu ya Mpiga Kura katika Uchaguzi Mdogo Jimbo la Kwahani

Imewekwa: 02 May, 2024
Tume yazialika taasisi na asasi za kiraia kutoa Elimu ya Mpiga Kura katika Uchaguzi Mdogo Jimbo la Kwahani

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetoa mwaliko kwa taasisi na asasi za kiraia zenye nia ya kutoa elimu ya mpiga kura katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Kwahani.

 

Mwaliko huo umetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima, R. K kufuatia taarifa kwa umma kuhusu uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Kwahani lililopo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar, utakaofanyika siku ya Jumamosi tarehe 08 Juni, 2024.

 

Alisema mwaliko huo unatokana na kifungu cha 10(1)(g) na (h) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024, kinachoipa mamlaka Tume kutoa elimu ya mpiga kura nchini, kuratibu na kusimamia taasisi na asasi za kiraia zinazotoa elimu hiyo.

 

“Hivyo, kupitia tangazo hili, Tume inakaribisha maombi kutoka taasisi na asasi za kiraia nchini zenye nia ya kutoa elimu ya mpiga kura katika uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la Kwahani.” Alisema Bw. Kailima na kuongeza kuwa:

 

“Taasisi na asasi za kiraia zenye nia ya kutoa elimu ya mpiga kura zinatakiwa kuwasilisha maombi yao kwa njia ya barua pepe: info@inec.go.tz au uchaguzi@inec.go.tz. Maombi hayo yatapokelewa kuanzia tarehe 02  hadi  tarehe 07 Mei, 2024.”

Kwa mujibu wa mwaliko huo, barua ya maombi inatakiwa kuainisha mambo yafuatayo kuhusu taasisi au asasi husika. Iwe imesajiliwa kwa mujibu wa Sheria za Tanzania, iwe imefanya kazi nchini kwa kipindi kisichopungua miezi sita tangu kusajiliwa kwake na ikiwa taasisi au asasi ya kiraia inahusisha watendaji wa kimataifa, miongoni mwa watendaji wake wakuu, wawili ambao taarifa zao zitawasilishwa wanapaswa wawe Watanzania.

 

Jambo lingine ni kwamba taasisi au asasi husika katika utendaji wake, iwe haijahusishwa na uchochezi au kuvuruga amani, iwe na uzoefu wa kutoa elimu ya mpiga kura; na iwe tayari kujigharamia katika kutoa elimu ya mpiga kura.

 

Mwaliko huo umeitaka taasisi au asasi inayotaka kutoa elimu hiyo kuambatisha nakala au kivuli cha cheti cha usajili, nakala au kivuli cha Katiba ya taasisi au asasi ya kiraia na majina matatu ya viongozi wa juu wa taasisi au asasi ya kiraia.

 

Kiambatisho kingine ni anuani kamili ya makazi na namba za simu za ofisi na za viongozi wake na ratiba itakayoonesha tarehe na mahali elimu ya mpiga kura itakapotolewa katika wilaya husika.

 

Imesisitiza mwaliko huo kuwa, Tume haitahusika na utoaji wa rasilimali fedha au rasilimali nyingine kwa ajili ya kugharamia zoezi la utoaji wa elimu ya mpiga kura kwa taasisi au asasi za kiraia zitakazopewa kibali.