Tume yazialika taasisi na asasi zinazotaka kutazama Uchaguzi Mdogo wa Madiwani katika Kata 23

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekaribisha maombi kutoka taasisi na asasi mbalimbali nchini zinazohitaji kutazama uchaguzi mdogo katika kata 23 zilizopo halmashauri mbalimbali nchini utakaofanyika siku ya Jumatano tarehe 20 Machi mwaka 2024.
Kata zinazofanya uchaguzi ni Kimbiji iliyopo (Kigamboni Mc), Kasingirima (Kigoma/Ujiji Mc), Ndevelwa (Tabora Mc), Msangani (Kibaha Tc), Utiri (Mbinga Tc), Fukayosi (Bagamoyo Dc), Mlanzi (Kibiti Dc), Mbingamhalule (Songea Dc), Isebya (Mbogwe Dc), Kibata (Kilwa Dc), Mshikamano (Musoma Mc), Na Kata Ya Busegwe Iliyopo (Butiama Dc),
Nyingine ni Kata ya Nkokwa iliyopo (Kyela Dc), Kamwene (Mlimba Dc), Chipuputa (Nanyumbu Dc), Buzilasoga (Sengerema Dc), Mhande (Kwimba Dc), Kabwe (Nkasi Dc), Bukundi (Meatu Dc), Mkuzi (Muheza Dc) na Kata za Boma, Mtimbwani na Mayomboni zilizopo (Mkinga Dc).
Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima, R. K taasisi na asasi zenye nia ya kutazama uchaguzi huo ziwasilishe maombi kwa kutumia anuani (link) ifuatayo https://oms.nec.go.tz
Barua ya maombi pamoja na mambo mengine itatakiwa kuainisha mambo yafuatayo:-
i. Anuani kamili ya taasisi au asasi husika;
ii. Mahali ambapo taasisi au asasi husika inafanyia kazi (Physical address);
iii. Shughuli ambazo zinafanywa na taasisi au asasi husika kwa mujibu wa hati ya usajili;
iv. Maeneo ambayo taasisi au asasi inapenda kwenda kutazama uchaguzi;
v. Idadi ya watu ambao taasisi au asasi itawatumia katika zoezi hilo pamoja na majina na taarifa zao binafsi;
vi. Majina na namba za simu za viongozi wa taasisi au asasi husika kama yalivyoandikwa katika hati za usajili;
vii. Ikiwa taasisi au asasi inahusisha watendaji wa kimataifa, viongozi wawili ambao taarifa zao zitawasilishwa ni lazima wawe watanzania;
viii. Kuambatisha nakala au kivuli cha hati ya usajili wa taasisi au asasi husika; na
ix. Kuambatisha nakala au kivuli cha katiba ya taasisi au asasi husika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo maombi ya kutazama uchaguzi yatapokelewa kuanzia tarehe 15 hadi 21 Februari, 2024.