Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Uchaguzi wa Ubunge katika Jimbo la Fuoni Wilaya ya Magharibi B, Zanzibar na Uchaguzi wa Udiwani katika Kata ya Chamwino Jimbo la Morogoro Mjini na Kata ya Mbagala Kuu Jimbo la Mbagala

Imewekwa: 03 Oct, 2025
Uchaguzi wa Ubunge katika Jimbo la Fuoni Wilaya ya Magharibi B, Zanzibar na Uchaguzi wa Udiwani katika Kata ya Chamwino Jimbo la Morogoro Mjini na Kata ya Mbagala Kuu Jimbo la Mbagala

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea taarifa kuhusu kifo cha mgombea wa ubunge mmoja na vifo vya wagombea udiwani watatu kama ifuatavyo:

  1. Kifo cha Ndugu Abass Ali Mwinyi, aliyekuwa mgombe wa Ubunge Jimbo la Fuoni Wilaya ya Magharibi B, Zanzibar, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kichotokea tarehe 25 Septemba, 2025. Uchaguzi katika Jimbo hilo ulisitishwa rasmi tarehe 25 Septemba, 2025.
  2. Kifo cha Ndugu Hassani Salum Hassani, aliyekuwa mgombea wa Udiwani katika Kata ya Chamwino, Jimbo la Morogoro Mjini kupitia Chama cha Civic United Front (CUF - Chama cha Wananchi) kilichotokea tarehe 27 Septemba, 2025. Uchaguzi katika Kata hiyo ulisitiwa rasmi tarehe 27 Septemba, 2025
  3. Kifo cha Ndugu Rajabu Sultan Mwanga, aliyekuwa mgombea Udiwani Kata ya Mbagala Kuu, Jimbo la Mbagala kupitia Chama cha Civic United Front (CUF - Chama cha Wananchi) kilichotokea tarehe 27 Septemba, 2025. Uchaguzi katika Kata hiyo ulisitiwa rasmi tarehe 29 Septemba, 2025

Hivyo, kutokana na vifo vya waliokuwa wagombea tajwa na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 68(1), (3) na (4) na 71(2) vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya Mwaka 2024, Tume inatoa taarifa kwa umma kuhusu ratiba ya uchaguzi wa Ubunge katika Jimbo la Fuoni na uchaguzi wa Udiwani katika Kata ya Chamwino na Kata ya Mbagala Kuu kama ifuatavyo: -

 

  1. Fomu za uteuzi kwa mgombea Ubunge Jimbo la Fuoni kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) na wagombea Udiwani katika Kata ya Chamwino na Kata ya Mbagala Kuu kupitia Chama cha Civic United Front (CUF - Chama cha Wananchi) zitatolewa kuanzia tarehe 15 Oktoba, 2025 hadi 21 Oktoba, 2025;
  2. Uteuzi wa mgombea Ubunge Jimbo la Fuoni na wagombea Udiwani katika Kata ya Chamwino na Kata ya Mbagala Kuu utafanyika tarehe 21 Oktoba, 2025;
  3. Kampeni za uchaguzi wa Ubunge Jimbo la Fuoni zitafanyika kama ifuatavyo: -
  1. Kampeni zitafanyika kuanzia tarehe 22 Oktoba, 2025 hadi 27 Oktoba, 2025,
  2. Tarehe 28 Oktoba, 2025 hadi 04 Novemba, 2025 kampeni zitasitishwa ili kupisha upigaji kura ya mapema kwa upande wa Tanzania Zanzibar na siku ya kupiga kura hadi kutangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, na
  3. Tarehe 05 Novemba, 2025 hadi tarehe 29 Desemba, 2025 kampeni zitaendelea.
  1. Kampeni za uchaguzi wa Udiwani katika Kata ya Chamwino na Kata ya Mbagala Kuu zitafanyika kama ifuatavyo: -
  1. Kampeni zitafanyika kuanzia tarehe 22 Oktoba, 2025 hadi 28 Oktoba, 2025,
  2. Tarehe 29 Oktoba, 2025 hadi 04 Novemba, 2025 kampeni zitasitishwa ili kupisha siku ya kupiga kura hadi kutangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, na
  3. Tarehe 05 Novemba, 2025 hadi tarehe 29 Desemba, 2025 kampeni zitaendelea.
  1. Uchaguzi wa Ubunge Jimbo la Fuoni na Udiwani katika Kata ya Chamwino na Kata ya Mbagala Kuu utafanyika siku ya Jumanne tarehe 30 Desemba, 2025.

Aidha, kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 71(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Na. 1 ya mwaka 2024, uteuzi mpya hautahusisha mgombea mwingine yeyote aliyeteuliwa kihalali katika uteuzi uliofanyika awali isipokuwa kama atatoa taarifa ya kujitoa.

Tume inatumia nafasi hii kuvikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na Maelekezo ya Tume katika kufanikisha ratiba ya uchaguzi husika.

Imetolewa na:

 

Kailima, R. K

MKURUGENZI WA UCHAGUZI

 

“KURA YAKO HAKI YAKO JITOKEZE KUPIGA KURA”