Uteuzi wa wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wabunge kwa Jamhuri ya Muungano na Madiwani kwa Tanzania Bara

Kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 34(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, kikisomwa pamoja na kanuni ya 20(1) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025 na Ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ilianza kutoa fomu za uteuzi kwa wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 09 Agosti, 2025 na zoezi hilo linatarajiwa kukamilika kesho tarehe 27 Agosti, 2025, ambayo ndiyo siku ya uteuzi.
Zoezi la urejeshaji wa fomu na uteuzi wa wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais litafanyika katika ofisi za Tume zilizopo eneo la Njedengwa - Dodoma kuanzia saa 1:30 Asubuhi hadi saa 10:00 Alasiri.
Kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 50 na 62 vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, vikisomwa pamoja na kanuni ya 23 na 26 za Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025, uteuzi wa wagombea Ubunge kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani kwa Tanzania Bara utafanywa na wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi katika ngazi ya jimbo kwa wagombea ubunge na ngazi ya kata kwa wagombea udiwani. Uteuzi utafanyika kesho tarehe 27 Agosti, 2025 kuanzia saa 1:30 Asubuhi hadi saa 10:00 Alasiri.
Maandalizi yote kwa ajili ya zoezi la uteuzi wa wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais, wagombea Ubunge na Udiwani yamekamilika, hivyo, Tume inawahimiza wagombea waliochukua fomu za uteuzi kwa ajili ya Kiti cha Rais na Makamu wa Rais kufika katika ofisi za Tume Dodoma na wagombea waliochukuwa fomu kwa ajili ya uteuzi wa nafasi za ubunge na udiwani kufika katika ofisi za wasimamizi wa uchaguzi au wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kwa wakati ili kuwasilisha fomu zao za uteuzi.
Baada ya kukamilika kwa zoezi la uteuzi saa 10:00 Alasiri Fomu za wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais zitabandikwa katika mbao za matangazo nje ya ofisi ya Tume kwa ajili ya ukaguzi. Aidha, fomu za wagombea wa Ubunge zitabandikwa katika mbao za matangazo nje ya ofisi za wasimamizi wa uchaguzi na fomu za wagombea Udiwani zitabandikwa nje ya ofisi za wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi.
Tunavisihi vyama vya siasa na wanaopendekezwa kugombea kuzingatia maelezo na maelekezo yaliyoainishwa katika barua tulizowatumia kuwajulisha muda wa kuwasilisha fomu.
"KURA YAKO HAKI YAKO JITOKEZE KUPIGA KỰRA"
Imetolewa na Kailima, R.K MKURUGENŻI WA UCHAGUZI