Utoaji wa Fomu za Uteuzi wa Wagombea Ubunge kwa Jamhuri ya Muungano na Udiwani kwa Tanzania Bara

Mnamo tarehe 26 Julai, 2025, kwa kuzingatia masharti ya ibara ya 41(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na kifungu cha 41(1) na 49(1) vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza Ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025.
Ratiba hiyo ilionesha tarehe za utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea wa nafasi ya Ubunge kwa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania na Madiwani kwa Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa Ratiba ya Uchaguzi Mkuu iliyotangazwa na Tume na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 50(6) na kifungu cha 62 (6) vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, vikisomwa pamoja na kanuni ya 23 na 26 za Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025, kuanzia leo tarehe 14 Agosti, 2025 hadi tarehe 27 Agosti, 2025 Wasimamizi wa Uchaguzi wa majimbo wataanza kutoa fomu za uteuzi wa wagombea Ubunge katika Jamhuri ya Muungano na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya kata wataanza kutoa fomu za uteuzi wa wagombea Udiwani kwa Tanzania Bara.
Hivyo, wanachama wa vyama vya siasa waliopendekezwa na vyama vyao kugombea nafasi ya Ubunge kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wafike katika ofisi za Wasimamizi wa uchaguzi wakiwa na barua za utambulisho kutoka 1 B katika vyama vyao kuanzia saa moja na nusu (1:30) asubuhi hadi saa kumi kamili (10:00) alasiri.
Aidha, kwa wanachama waliopendekezwa kugombea nafasi ya Udiwani kwa Tanzania Bara wafike katika ofisi za Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya kata wakiwa na barua za utambulisho kutoka katika vyama vyao kuanzia saa moja na nusu (1:30) asubuhi hadi saa kumi kamili (10:00) Alasiri.
Tume inavipongeza vyama vyote vya siasa kwa kuendelea kufanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Tume kwa upande wake itazingatia Katiba, sheria na kanuni wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.
"KURA YAKO HAKI YAKO JITOKEZEKUPIGA KURA"