Vyama nane vyateuliwa kuwania kiti cha Udiwani Kata ya Bukundi

Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Bukundi katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu Bw. Richard Masanja Chalya amefanya uteuzi wa wagombea kutoka vyama nane vya siasa kushiriki Uchaguzi Mdogo wa Udiwani wa kata hiyo utakaofanyika tarehe 20 Machi, 2024.
Akizungumza baada ya uteuzi Bw. Chalya amesema wagombea wote nane waliochukua fomu za uteuzi kuanzia tarehe 27 Februari, 2024 wamekidhi sifa na masharti ya uteuzi na hivyo wameteuliwa kugombea Udiwani katika Kata yaBukundi.
Wagombea waliochukua fomu za uteuzi na kufanikiwa kuteuliwa niBw. Tilusubya Mgana Mwangwa (Demokrasia Makini) Bw. Majengo Mohamed Ntandu (AAFP ), Bw. Paurini Richard Mayila (ACT-Wazalendo), Bi. Kweji Sylvester Mpella (NLD) na Bw.Yunus Kilo Ally wa CCM.
Wengine ni Bw. Robert Mashaka Igonji wa United People's Democratic Party (UPDP), Bw. Joseph Masibuka Nzagwina wa Chama cha Union for Multi-Party Democracy (UMD) na mgombeq Bw. Ngasa Shija Masanja wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU).
Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 23 za Tanzania Bara zitaanza tarehe 5 hadi 19 Machi, 2024 na siku ya uchaguzi itakuwa tarehe 20 Machi, 2024.
Mbali na Kata ya Bukundi, kata nyingine zinazofanya uchaguzi huo ni ni Isebya (Mbogwe DC), Kibata (Kilwa DC), Mshikamano (Musoma MC), Busegwe (Butiama DC), Nkokwa (Kyela DC), Kamwene (Mlimba DC), Chipuputa (Nanyumbu DC), na kata ya Buzilasoga (Sengerema DC).
Nyingine ni Kata ya Mhande (Kwimba DC), Kabwe (Nkasi DC), Bukundi (Kigamboni MC) Mkuzi (Muheza DC) na kata za Boma, Mtimbwani na Mayomboni (Mkinga DC).