Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Wadau wa Uchaguzi mikoa ya Arusha, Kilimanjaro waaswa kushiriki uboreshaji wa Daftari kuanzia tarehe 11 hadi 17 Desemba 2024

Imewekwa: 29 Nov, 2024
Wadau wa Uchaguzi mikoa ya Arusha, Kilimanjaro waaswa kushiriki uboreshaji wa Daftari kuanzia tarehe 11 hadi 17 Desemba 2024

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,  Jaji wa Mahakama ya  Rufaa Mh. Jacobs Mwambegele amefungua mkutano wa Tume na wadau wa uchaguzi uliofavyika Jijini Arusha ikiwa ni maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mzunguko wa saba.

Akifungua mkutano Mhe. Mwembegele amesema uboreshaji huo utahusisha mikoa ya Arusha, Kilimamnjaro na halmashauri za wilaya ya Chemba, Kondoa na Mji wa Kondoa katika Mkoa wa Dodoma na utafanyika kuanzia tarehe 11 hadi 17 Desemba, 2024.

Ametoa rai kwa viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, wazee wa kimila, asasi za kiraia zinazowakilisha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, kutumia majukwaa yao kuwahimiza wananchi wa mkoa huo ili wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Naye Makamu Mweneyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,  Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa Mh. Mbarouk Salim Mbarouk akifungua mkutano wa Tume na wadau wa uchaguzi wa Mkao wa Kilimanjaro amewakumbusha wadau hao kuwa kadi za mpiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 zenye jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni halali na zitaendelea kutumika kwenye chaguzi zijazo.

“Hivyo, zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura haliwahusu wapiga kura wenye kadi hizo na ambao kadi zao hazijaharibika au kupotea au hawajahama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo jingine au kuboresha taarifa zao.” amesema Jaji Mst. Mbarouk.

 Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhan amesema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia Gazeti la Serikali Na. 796 lililotolewa tarehe 6 Septemba, 2024 ametangaza kurejesha maeneo ya kiutawala yaliyokuwa yamefutwa awali ikiwemo kata 11 za Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.

“Hivyo, Tume imeridhia kufanya mabadiliko ya vituo vya kuandikisha wapiga kura kutoka vituo 40,126 vya awali  hadi kufikia vituo 40,170 kwa kurejesha vituo 44 vya kata 11 za Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwa ajili ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura” amesema Bw. Kailima.

Katika uboreshaji huo  vituo vya kuandikisha wapiga kura vitakuwa katika mitaa, vijiji na vitongoji na vitafunguliwa saa 2 kamili asubuhi na kufungwa saa 12 kamili jioni. Kaulimbiu ya uboreshaji huo inasema ‘Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora’.