Wadau wa Uchaguzi Njombe watakiwa kutumia majukwaa yao kuwahimiza wananchi kujiandikisha, kuboresha na kuhamisha taarifa zao
Wadau wa Uchaguzi Mkoa wa Njombe wametakiwa kutumia majukwaa yao ya kisiasa , kijamii, kitamaduni na kuichumi kuwahimiza wananchi wa mkoa huo wajitokeze kwa wingi kujiandikisha, kuboresha na kuhamisha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele katika hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Wadau wa Uchaguzi Mkoa wa Njombe iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Hududma za Sheria wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Selemani Mtibora.
Amesema kufanikiwa kwa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Mkoa wa Njombe, kunategemea sana ushiriki wao katika kutoa elimu ya mpiga kura na kuhamasisha wananchi wenye sifa wajitokeze kwa wingi kuandikishwa, kuboresha na kuhamisha taarifa zao.
Amewahakikishia wadau hao kuwa, Tume inathamini sana uwepo wao kwa kuwa ni sehemu ya mafanikio ya uboreshaji wa Daftari na kwamba Tume ina imani itaendelea kupata ushirikiano mkubwa zaidi kutoka kwao na watatumia nafasi zao kwa jamii kuwafikia wananchi wa Mkoa wa Njombe.
“Kwa mujibu wa ratiba, kwa sasa Tume imeanza maandalizi ya mzunguko wa tisa kati ya mizunguko 13 ya uboreshaji wa Daftari. Aidha, mzunguko huu wa tisa unahusisha mikoa minne ya Njombe hapa tulipo leo na mikoa ya Songwe, Rukwa na sehemu ya Mkoa wa Ruvuma kwenye Halmashauri za Wilaya ya Nyasa, Mbinga, Mbinga Mji, Wilaya ya Songea na Manispaa ya Songea.” amesema Jaji (Rufaa) Mwambegele.
Mbali na kusisitiza hayo, Jaji (Rufaa) Mwambegele amewakumbusha wadau hao na wananchi kuwa kujiandikisha kuwa mpiga kura zaidi ya zaidi ya mara moja ni kutenda kosa la jinai na atakayetiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua Shilingi 100,000 na isiyozidi Shilingi 300,000 au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili gerezani au vyote kwa pamoja.
“Hivyo, natumia fursa hii kuwaasa wananchi kujiepusha na kosa la kujiandikisha zaidi ya mara moja na niwaombe wadau mliopo hapa mkawaelimishe wananchi kwamba wakajiandikishe mara moja na kwenye kituo kimoja ili kuepuka uvunjaji wa sheria”, amesema Jaji (Rufaa) Mwambegele.
Lengo la mkutano wa Tume na wadau wa uchaguzi ni kupeana taarifa kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Tume ikiwemo maandalizi, mifumo ya uandikishaji, vituo vya kuandikisha wapiga kura ili kufanikisha zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura katika mzunguko wa tisa unatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 12 hadi 18 Januari, 2025 na Kaulimbiu ya uboreshaji ni “Kujiandikisha kuwa Mpiga Kura Ni Msingi wa Uchaguzi Bora”.