Watendaji wa uboreshaji wa Daftari ngazi ya kata wilayani Ruangwa watakiwa kutumia lugha nzuri kuwahudumia wananchi

Maafisa Waandikishaji Wasidizi na Waendesha Kifaa cha Bayometriki wa kata za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mkoa wa Lindi wametakiwa kutumia lugha nzuri kwa wananchi wanaofika kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura wakati wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Mahakama Kuu Asina Omari, wakati alipotembelea mafunzo kwa watendaji hao ikiwa ni maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudmu la Wapiga Kura.
Mhe. Jaji Asina amewasisitiza watendaji hao wawasisitize watendaji ngazi ya vituo watumie lugha nzuri kwa wateja hasa pale mpiga kura aliyejiandikisha anapofika kituoni kuhakiki taarifa zake akiwa na kadi yake ya mpiga kura.
Amemuomba Afisa Mwandikishaji kusisitiza matumizi ya lugha nzuri kwa wateja kwenye mafunzo ya watendaji wa vituo kwani inawezekana mpiga kura akafika kituoni na kupanga foleni ili ahakiki kadi yake yake, hivyo ni vyema akahudumiwa kwa lugha nzuri.
Aidha, Mhe. Jaji Asina amewataka watendaji hao wa uboreshaji wa Daftari ngazi ya kata kutumia majukwaa waliyonayo kuwaelimisha na kuhamasisha wananchi kwenye kata zao kwenda kujiandikisha au kuboresha taarifa zao wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Kwa upande wake Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Magdalena Rwebangira amezungumza na washiriki wa mafunzo ya uboreshaji wa Daftari kwa maafisa waandikishaji wasaidizi ngazi ya kata na waendesha kifa cha Bayometriki katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoa wa Ruvuma.
Ameawataka watendaji hao kuzingatia yale wanayofundishwa na kwa kutambua umuhimu wa mafunzo hayo kwani hitilafu yoyote inayotokea kwenye uboreshaji wa Daftari, inaweza kusababisha utekelezaji wa jukumu la uboreshaji kuzorota.
“Kwa hiyo niwasihi sana mfanye kazi yenu kwa weledi ili kuwepo na mwitikio mzuri wa wananchi kushiriki katika kujiandikisha au kuboreshaji taarifa zao. Na weledi wenyewe ni kuzingatia mtakayojifunza na kuwasisitiza watendaji wa vituo mtakaowafundisha wawe makini na kufanya kazi katika siku zote saba kama inavyoelekezwa” amesema Mhe. Rwebangira.
Uboreshaji wa Daftari la Kudmu la Wapiga Kura unatarajiwa kufanyika katika mikoa ya Mtwara, Lindi na halamshauri za wilaya ya Madaba, Namtumbo na Tunduru katika Mkoa wa Ruvuma kuanzia tarehe 28 Januari hadi tarehe 03 Februari, 2025.