Watendaji wa uboreshaji wa Daftari Zanzibar watakiwa kuzingatia Katiba ya nchi, sheria za Uchaguzi kutekeleza majukumu yao
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Balozi Omari Ramadhan Mapuri amewataka watendaji wa uboreshaji wa Daftari Zanzibar kuzingatia Katiba ya nchi, sheria za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na kanuni zake katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mhe. Balozi Mapuri ameyasema hayo leo tarehe 02 Oktoba, 2024 wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi na Maafisa TEHAMA kisiwani Pemba.
Amewahimiza watendaji hao kuwahamasisha wananchi wenye sifa wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi wao.
“Ni matarajio ya Tume kuwa, mara baada ya zoezi hili kukamilika watu watakaokuwa wamepatiwa kadi watakuwa ni wapiga kura halali wa kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” amesema Mhe. Balozi Mapuri.
Kwa upande wake Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Magdalena Rwebangira amewataka watendaji hao kutekeleza jukumu la kuhamasisha wananchi wa maeneo yao kushiriki kwenye uboreshaji kwa kushirikiana na wadau wengine wa uchaguzi.
“Mabango na vipeperushi mtakavyopewa na Tume mvisambaze mapema katika shehia zote zilizopo katika mikoa yote mitatu ya Unguja. Kazi yenu kubwa ni kusimamia na kuendesha shughuli zote za uboreshaji katika shehia zote” amesema Mhe. Magdalena.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura visiwani Zanzibar umepangwa kufanyika kuanzia tarehe 7 hadi 13 Oktoba, 2024 ambapo katika Ksiwa cha Pemba utafanyika katika mikoa miwili na Unguja katika mikoa mitatu.