Watendaji wa uboreshaji Zanzibar watakiwa kuzingatia weledi kufanikisha uboreshaji wa Daftari visiwani Zanzibar
Watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Zanzibar wametakiwa kufanya kazi kwa weledi, bidi na moyo wa kujituma ili kufanikisha zoezi hilo linalotarajiwa kufanyika visiwani humo kuanzia tarehe 7 hadi 13 Oktoba, 2024.
Hayo yamesemwa leo na Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Rufaa Mst. Mbarouk Salim Mbarouk wakati akifungua mafunzo kwa Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi na Maafisa TEHAMA kisiwani Pemba.
Mhe. Jaji Mst. Mbarouk amesema mbali na kufanya kazi kwa weledi na kujituma, amewataka baadhi ya watendaji hao waliopata uzoefu wa kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Tume ikiwemo uboreshaji wa Daftari, kutumia uzoefu huo kuwasidia wenzao ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Kuhusu kuwashirikisha wadau, Mhe Jaji wa Rufaa Mst. Mbarouk, alisisitiza kuwashirikisha mawakala wa vyama vya siasa watakaoruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura kwani kutasaidia kuleta uwazi katika zoezi la uboreshaji wa Daftari kwani mawakala watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo, kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima.
“Mawakala au viongozi wa vyama vya siasa hawaruhusiwi kuingilia mchakato wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kituoni” amesema Mhe. Jaji wa Rufaa Mst. Mbarouk.
Kwa upande wake Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Mahakama Kuu Asina Omari amefungua mafunzo kwa watendaji wa uboreshaji, yanayofanyika kisiwani Unguja na kuwataka watendaji hao kutekeleza majukumu yao kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji hasa ikizingatiwa kuwa vifaa hivyo vimenunuliwa kwa gharama kubwa.