Yunusi Kilo Ally aibuka mshindi Uchaguzi Mdogo wa Udiwani Kata ya Bukundi

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Meatu Bw. Athumani Masasi amemtangaza Bw. Yunusi Kilo Ally wa CCM kuwa mshindi wa Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika Kata ya Bukundi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu uliofanyika tarehe 20 Machi, 2024, kwa kupata kura 2,182 akimshinda Bw. Joseph Masibuka Nzagwina wa UMD aliyepata kura 422.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Bw. Masasi alisema Ngassa Shija Masanja wa Chama cha SAU alipata kura 34, Bw. Tirusubya Mgana Mwangwa wa Chama cha Demokrasia Makini alipata kura 28, Bw. Majengo Mohamed Ntandu wa Chama cha AAFP alipata kyura 22.
Aliongeza kuwa Bw. Paurini Richard Mayila wa Chama cha ACT-Wazalendo alipata kura 9, Bw. Robert Mashaka Igonji wa Chama cha UPDP alipata kura 4 na mgombea pekee mwanamke katika uchaguzi huo Bi. Kweji Sylivester Mpella wa Chama cha NLD akipata kura 3.
Baada ya kutangazwa matokeo hayo, mgombea wa NLD Bi. Kweji Mpella alitoa shukra kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kurartibu na kusimamia uchaguzi huo kwa kuzingatia sheria na kutoa ushirikiano mkubwa kwa wagombea tangu wakati wa uteuzi.
Kwa upande wake mgombea wa AAFP Bw. Majengo Mohamed Ntandu alimpongeza mshindi wa uchaguzi huo huo na kumtaka akawatumikie wananchi wa Bukundi huku akitoa shukrani kwa wasimamizi wa uchaguzi kwa usimamizi mzuri wa uchaguzi huo.
Naye Diwani Mteule wa Kata ya Bukundi Bw. Yunusi Kilo Ally alitoa shukrani kwa kufanikiwa kuongozakatika uchaguzi huo.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Meatu Bw. Athumani Masasi alimkabidhi Hati ya Ushindi Bw. Yunusi Kilo Ally wa CCM baada ya kuibuka mshindi wa Udiwani katika Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika Kata ya Bukundi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu.
Kata ya Bukundi ni miongoni mwa kata 22 za Tanzania Bara zilizofanya Uchaguzi Mdogo wa Udiwani uli uliofanyika tarehe 20 Machi, 2024.
Kata nyingine zilizofanya uchaguzi huo ni Kimbiji (Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni), Kasingirima (Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji), Ndevelwa (Halmashauri ya Manispaa ya Tabora), Msangani (Halmashauri ya Mji Kibaha), Fukayosi(Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo), Mlanzi (Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti), Utiri (Halmashauri ya Mji Mbinga) na Mbingamhalule (Halmashauri ya Wilaya ya Songea).
Nyingine ni Isebya (Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe), Kibata (Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa), Mshikamano (Halmashauri ya Manispaa ya Musoma), Busegwe (Halmashauri ya Wilaya ya Butiama), Nkokwa (Halmashauri ya Wilaya ya Kyela), Kamwene (Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba), Chipuputa (Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu), Buzilasoga (Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema), Mhande (Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba), Kabwe (Halmashauri ya Nkasi), Mkuzi (Halmashauri ya Wilaya ya Muheza) na kata za Boma, Mtimbwani na Mayomboni (Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga).