Wagombea Ubunge
Sifa za Mgombea Ubunge
Kwa mujibu wa Ibara ya 67 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge endapo: -
(i) Ni raia wa Jamhuri ya Muungano;
(ii) Ametimiza umri wa miaka ishirini na moja (21);
(iii) Anajua kusoma na kuandika kwa Kiswahili au Kiingereza;
(iv) Ni Mwanachama na mgombea aliyependekezwa na Chama cha siasa; na;
(v) Hajawahi kutiwa hatiani na Mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yoyote ya Serikali katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya uchaguzi.
Kukosa Sifa za Kugombea Ubunge
Ibara ya 67 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inaelekeza kuwa mtu hataruhusiwa kugombea Ubunge ikiwa:-
(i) Ni raia wa nchi nyingine; (ii)
Kwa mujibu wa Sheria inayotumika katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imethibitishwa rasmi kwamba mtu huyo ana ugonjwa wa akili;
(iii) Amehukumiwa na Mahakama yoyote katika Jamhuri ya Muungano na kupewa adhabu ya kifo au ya kufungwa gerezani kwa muda unaozidi miezi sita kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote, vyovyote linavyoitwa, linaloambatana na utovu wa uaminifu;
(iv) Katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu amehukumiwa na kupewa adhabu ya kifungo kwa kosa linaloambatana na utovu wa uaminifu au kwa kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma;
(v) Mtu huyo si Mwanachama wa Chama cha Siasa na ambaye hajapendekezwa na Chama cha Siasa kuwa Mgombea;
(vi) Mtu huyo ana maslahi yoyote katika mkataba wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wa aina yoyote aliyowekewa miiko maalum kwa Mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge, na iwapo amekiuka miiko hiyo;
(vii) Ameshika madaraka ya Afisa Mwandamizi katika Utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, isipokuwa madaraka ambayo Rais anaweza au anatakiwa kukabidhi kwa Mbunge kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano au Sheria iliyotungwa na Bunge;
(viii) Kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge inayoshughulikia makosa yanayohusika na uchaguzi wa aina yoyote, mtu huyo amezuiliwa kujiandikisha kama mpiga kura au kupiga kura katika uchaguzi wa Wabunge; na
(ix) Ni mgombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mtu aliyepewa adhabu ya kulipa faini au kifungo na akalipa faini hazuiwi kugombea Ubunge. Iwapo atapewa adhabu ya kulipa faini akashindwa na akatumikia kifungo na kukimaliza kabla ya siku ya uteuzi anaruhusiwa kugombea. Hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 67 (7)(a) na (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, 1977. Kiongozi wa Chama cha Siasa haruhusiwi kupendekeza jina lake na kujidhamini mwenyewe.
Masharti ya Uteuzi wa Mgombea Ubunge
Masharti ya uteuzi wa Wagombea Ubunge ni kama ifuatavyo:-
(i) Adhaminiwe na wapiga kura wasiopungua ishirini na tano (25) walioandikishwa kuwa wapiga kura katika Jimbo linalohusika. Mgombea haruhusiwi kujidhamini yeye mwenyewe. Mpiga kura anatakiwa kudhamini mgombea Ubunge mmoja tu.
(ii) Awe ametoa tamko mbele ya Hakimu kuthibitisha kwamba anazo sifa zinazotakiwa kugombea Ubunge na hajapoteza sifa hizo.
(iii) Aweke dhamana ya shilingi elfu hamsini (50,000/=) kwa Msimamizi wa Uchaguzi kupitia akaunti ya amana ya Halmashauri atakayopatiwa siku akichukua fomu za uteuzi. Mgombea akishalipa atawasilisha pay-in slip ya benki kwa Msimamizi wa Uchaguzi ili apewe stakabadhi ya kukiri mapokezi. Ni muhimu kuhakikisha wagombea wanapewa akaunti namba ya amana ya Halmashauri kwa ajili ya malipo ya dhamana wanapochukua fomu za uteuzi.
Taratibu za Uteuzi wa Mgombea Ubunge
Mgombea hutakiwa kujaza Fomu namba 8B inayohusu taarifa zake binafsi, na zithibitishwe na Chama kilichomteua ngazi ya Mkoa, Wilaya au Jimbo kwamba ni za kweli. Mgombea awasilishe nakala nne (4) za fomu ya Uteuzi kwa Msimamizi wa Uchaguzi si zaidi ya saa kumi kamili (10:00) jioni siku ya Uteuzi. Fomu hizo ziwasilishwe pamoja na:-
(i) Picha nne za rangi (passport size) zenye ukubwa sawa na picha inayotumika katika hati ya kusafiria na ziandikwe majina kamili ya mgombea, Jimbo na Chama kwa nyuma.
(ii) Uthibitisho wa malipo ya dhamana ya shilingi elfu hamsini (50,000/=) (iii) Fomu Na. 10 ya tamko la kuheshimu na kutekeleza Maadili ya Uchaguzi. Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo, atabandika kwenye ubao wa matangazo mahali pa wazi nakala moja ya Fomu zote zenye picha za wagombea, baada ya saa kumi kamili (10.00) jioni siku ya Uteuzi mpaka saa kumi kamili (10.00) jioni siku inayofuata ili ziweze kukaguliwa.
Pingamizi dhidi ya Wagombea Ubunge
Pingamizi dhidi ya uteuzi wa Mgombea linalenga kuweka zuio kwa Mgombea ubunge aliyeteuliwa na Msimamizi wa Uchaguzi kwamba hana sifa za kuteuliwa kwa mujibu wa sheria. Pingamizi linaweza kuwekwa kuanzia saa 10:00 jioni siku ya uteuzi hadi saa 10:00 jioni siku inayofuatia baada ya siku ya uteuzi. 40 Kwa mujibu wa Kifungu cha 40 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 sababu ya pingamizi inaweza kuwa yoyote kati ya zifuatazo, kwamba mgombea:- (a) Si raia wa Tanzania;
(b) Hajatimiza umri wa miaka 21;
(c) Hana sifa za kuwa mgombea Ubunge;
(d) Hawezi kusoma na kuandika kwa Kiswahili au Kiingereza;
(e) Si Mwanachama wa Chama cha Siasa kilichosajiliwa kwa Mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa;
(f) Hakudhaminiwa na Chama cha Siasa kugombea Ubunge;
(g) Ametiwa hatiani kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yoyote ya Serikali katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi;
(h) Hakudhaminiwa na idadi ya Wapiga Kura inayotakiwa;
(i) Hakulipa dhamana ya shilingi elfu hamsini (50,000/=);
(j) Hajaambatisha picha katika fomu ya Uteuzi;
(k) Hakuwasilisha tamko la Kisheria;
(l) Hakutaja gharama na vyanzo vya fedha atakazotumia katika Uchaguzi chini ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi, Sura ya 278. (Pingamizi kuhusiana na sababu hii litawekwa na Msajili wa Vyama vya Siasa tu);
(m) Hajatoa Tamko la kuheshimu na kutekeleza Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2020;
(n) Hakurudisha fomu za uteuzi kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na sheria;
(o) Ametenda vitendo alivyokatazwa chini ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi, Sura ya 278 (Pingamizi kuhusiana na sababu hii litawekwa na Msajili wa Vyama vya Siasa tu); na 41
(p) Hakudhaminiwa na wapiga kura walioandikishwa katika Jimbo.
Muda wa Kuweka Pingamizi
Pingamizi dhidi ya Mgombea litawasilishwa kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata si zaidi ya saa kumi kamili (10:00) jioni siku ya inayofuatia baada ya siku ya uteuzi. Pingamizi litolewe kwa maandishi katika Fomu Na.9B litaje sababu na litiwe saini na muweka pingamizi. Wanaostahili kuwasilisha pingamizi hilo ni Mgombea mwingine wa nafasi hiyo, Msimamizi wa Uchaguzi au Mkurugenzi wa Uchaguzi.
Uamuzi wa Pingamizi na Rufaa
(i) Msimamizi wa Uchaguzi mara baada ya kupokea pingamizi atamtaarifu kwa maandishi Mgombea aliyepingwa na kumtaka atoe maelezo yake kabla ya kutoa uamuzi wa kukubali au kukataa pingamizi;
(ii) Kifungu cha 40 (6) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Na. 1 ya mwaka 1985 Sura ya 343, kinawaruhusu Wagombea kukata rufaa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupinga uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi kuhusu pingamizi dhidi ya Mgombea; Uamuzi wa rufaa za pingamizi utakaotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni wa mwisho na hautahojiwa mahakamani. Msajili wa Vyama vya Siasa atawasilisha pingamizi kwa Msimamizi wa Uchaguzi kwa kutumia fomu namba 9B si chini ya siku saba na si zaidi ya siku kumi na nne baada ya siku ya uteuzi.
Kukata Rufaa
Kifungu cha 40 (6) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, kinaruhusu wagombea kukata rufaa Tume kupinga uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi kuhusu pingamizi dhidi yao. Kwa utekelezaji bora wa suala hili, Tume imeweka masharti yafuatayo: - 42
(i) Rufaa dhidi ya maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi kuhusu uteuzi wa mgombea Ubunge zitatolewa kwa kujaza Fomu Na. 12, Tume itapeleka fomu hizo kwa Msimamizi wa Uchaguzi. Warufani watajaza nakala tatu (3) za fomu hizo.
(ii) Kwa mujibu wa Kanuni ya 31 (1) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2020, fomu ziwasilishwe kwa Msimamizi wa Uchaguzi katika muda wa saa ishirini na nne (24) tangu Msimamizi wa Uchaguzi alipotoa uamuzi unaopingwa.
(iii) Msimamizi wa Uchaguzi apokee rufaa hizo kwa niaba ya Tume. Baada ya kuzipokea aandike muda wa kupokea, azisaini na kugonga muhuri wa Msimamizi wa Uchaguzi. Msimamizi wa Uchaguzi ahakikishe kwamba: -
(a) Anaitaarifu Tume mara moja kwa njia yoyote ya haraka kuhusu kupokelewa kwa rufaa yoyote.
(b) Rufaa hizo zifikishwe Tume katika muda usiozidi siku nne (4) tangu siku ya uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi.
(c) Pamoja na rufaa hizo, awasilishe Fomu ya Uteuzi Na. 8B, Fomu ya Pingamizi Na. 9B na vielelezo vingine vinavyohusiana na rufaa hiyo. Rufaa yoyote itakayopokelewa na Msimamizi wa Uchaguzi au Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, lazima iwasilishwe Tume mara moja.