Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

NEC Logo

Wagombea Kiti cha Urais

Kifungu cha 30 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, kimeweka utaratibu unaopaswa kufuatwa ili mtu aweze kuteuliwa kuwa Mgombea wa Kiti cha Urais na Makamu wa Rais. Tume kwa kuzingatia Kanuni ya 37 (6) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2020, hufanya Uteuzi wa Wagombea wa nafasi ya Kiti cha Rais baada ya kujiridhisha kuwa Mgombea amejaza na kutimiza masharti ya ujazaji wa Fomu Na 8A. Aidha, Mgombea atajaza Fomu Na. 10 ya Maadili ya Uchaguzi.

Sifa za Wagombea wa Kiti cha Rais

Kwa mujibu wa ibara ya 39(1) na 47(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, sifa za mgombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais ni hizi zifuatavyo:-

(i) Awe ni raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

(ii) Awe ametimiza umri wa miaka Arobaini (40);

(iii) Awe Mwanachama na Mgombea aliyependekezwa na Chama cha Siasa;

(iv) Awe anazo sifa za kumwezesha kuwa Mbunge au Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi; na 32

(v) Katika kipindi cha miaka mitano kabla ya Uchaguzi Mkuu awe hajawahi kutiwa hatiani katika Mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yoyote ya Serikali.

Masharti ya Uteuzi wa Mgombea wa kiti cha Rais / Makamu wa Rais

Mgombea wa kiti cha Rais/Makamu wa Rais kwa mujibu wa Sheria ni lazima:-

(i) Awe amedhaminiwa na wapiga kura wasiopungua mia mbili (200) waliojiandikisha kupiga kura katika mkoa, kwa mikoa kumi na kati ya hiyo angalau mikoa miwili iwe ya Tanzania Zanzibar. Hii inamaanisha mgombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais anatakiwa kudhaminiwa na jumla ya wapiga kura wasiopungua 2000 kutoka mikoa 10.

(ii) Awe ameweka dhamana ya Shilingi milioni moja (1,000,000/=) kwa Tume kupitia akaunti ya amana atakayopatiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi siku ya kuchukua fomu za uteuzi. Mgombea akishalipia atawasilisha stakabadhi ya malipo (payin slip) ya benki kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi ili apatiwe stakabadhi ya kukiri mapokezi.

(iii) Awe ametoa Tamko mbele ya Jaji kwamba anazo sifa zinazotakiwa na hajapoteza sifa hizo.

Wadhamini wa Wagombea wa Kiti cha Rais Watakaowadhamini Wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais:

(i) Wawe wamejiandikisha kuwa Wapiga Kura katika mikoa hiyo;

(ii) Wawe hawajamdhamini mgombea mwingine yeyote wa kiti cha Rais/Makamu wa Rais;

(iii) Si lazima wawe wanachama wa chama kilichompendekeza; wala si lazima wawe wanachama wa chama chochote cha siasa; na

(iv) Wawe wamewadhamini Wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais kwa kutumia Fomu ya Uteuzi

Taratibu za Uteuzi wa Wagombea wa Kiti cha Rais/Makamu wa Rais

(i) Wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais watawasilisha rasmi nakala nne (4) za fomu zao moja kwa moja Tume. Tume ikishapokea fomu za uteuzi na kujiridhisha kuwa wagombea wanazo sifa za kugombea itawateua.

(ii) Wagombea watawasilisha picha nne za rangi (passport size) zenye ukubwa sawa na picha zinazotumika kwenye hati ya kusafiria zilizopigwa ndani ya miezi mitatu kabla ya siku ya uteuzi. Muonekano wa picha hizo kwa nyuma uwe wa rangi nyeupe (white background) na nyuma ya picha liandikwe jina kamili la mgombea na Chama anachokiwakilisha.

(iii) Wagombea watawasilisha stakabadhi ya malipo ya dhamana ya kiasi cha shilingi milioni moja (1,000,000/=) za Kitanzania atakayopewa kutoka Tume. (iv) Baada ya kuwasilisha fomu ya uteuzi, wagombea watatakiwa kutoa tamko la kuheshimu na kutekeleza Maadili ya Uchaguzi mbele ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kujaza Fomu Na. 10.

(v) Tume itabandika nakala moja ya Fomu ya Uteuzi (Fomu Na. 8A) yenye picha ya mgombea, stakabadhi ya malipo na tamko la kuheshimu na kutekeleza Maadili ya Uchaguzi (Fomu Na. 10) kwa Wagombea walioteuliwa si zaidi ya saa kumi (10:00) jioni siku ya Uteuzi ili ziweze kukaguliwa na iwapo kuna pingamizi liwasilishwe Tume kupitia Fomu Na. 9A. Fomu hiyo ibandikwe katika eneo la wazi.

(vi) Mgombea akitaka anaweza kuwasilisha fomu zake Tume kuanzia siku tatu (3) kabla ya siku ya uteuzi kwa ajili ya ukaguzi na pale ambapo pana dosari mgombea ataelekezwa kurekebisha 34 dosari hizo. Mgombea arudishiwe fomu zake mara baada ya kukaguliwa. Hata hivyo, uteuzi rasmi utafanywa siku iliyotangazwa na Tume, siku ambayo Tume itapaswa kupokea fomu husika kutoka kwa wagombea na kufanya uteuzi. Mgombea akiwasilisha picha (passport size) isiyo na muonekano wa rangi nyeupe (white background) ateuliwe. Hii haitakuwa sababu ya pingamizi kwa mujibu wa sheria.

Pingamizi dhidi ya Wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais

Pingamizi dhidi ya Uteuzi wa Mgombea linalenga kuweka zuio kwa Mgombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais aliyeteuliwa na Tume kwamba hana sifa za kuteuliwa kwa Mujibu wa Sheria. Wanaoruhusiwa kuweka pingamizi ni hawa wafuatao:-

(i) Mgombea yeyote wa Kiti cha Rais/Makamu wa Rais;

(ii) Mkurugenzi wa Uchaguzi; (iii) Msajili wa Vyama vya Siasa; na

(iv) Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Muda wa Kuweka Pingamizi Muda wa kuweka pingamizi ni kuanzia saa Kumi Kamili (10:00) jioni siku ya Uteuzi mpaka saa kumi kamili (10:00) jioni siku inayofuata. Pingamizi litolewe kwa maandishi katika Fomu Na. 9A litaje sababu na litiwe saini na muweka pingamizi.

Sababu za Pingamizi Sababu za Pingamizi dhidi ya mgombea zinaweza kuwa yoyote kati ya hizi zifuatazo:-

(a) Si raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano;

(b) Hajatimiza umri wa miaka arobaini;

(c) Hana sifa za kuwa Mgombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais;

(d) Hana sifa za kuwa Mbunge au Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi;

(e) Si Mwanachama wa Chama cha Siasa kilichosajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa;

(f) Hakudhaminiwa na Chama cha Siasa kugombea Kiti cha Rais na Makamu wa Rais;

(g) Ametiwa hatiani na Mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yoyote ya Serikali katika kipindi cha miaka mitano (5) kabla ya uchaguzi; (h) Hakudhaminiwa na Wapiga Kura walioandikishwa katika Mikoa 10 ya Jamhuri ya Muungano, ikiwemo angalau Mikoa 2 ya Tanzania Zanzibar;

(i) Hakudhaminiwa na idadi ya wapiga kura inayotakiwa;

(j) Hakulipa dhamana ya shilingi milioni moja (1,000,000/=) za Kitanzania;

(k) Hajaambatisha picha kwenye fomu za Uteuzi;

(l) Hakutoa tamko la Kisheria kwa Mujibu wa Kifungu cha (4)(a) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343;

(m) Hakutaja gharama na vyanzo vya fedha atakazotumia katika uchaguzi chini ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi, Sura ya 278. (Pingamizi kuhusiana na sababu hii litawekwa na Msajili wa Vyama vya Siasa tu);

(n) Hakurudisha fomu za Uteuzi kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na Sheria;

(o) Hajatoa tamko la kuheshimu na kutekeleza Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2020; na

(p) Ametenda vitendo vilivyokatazwa chini ya Sheria ya Gharama ya Uchaguzi, Sura ya 278. (Pingamizi kuhusiana na sababu hii litawekwa na Msajili wa Vyama vya Siasa tu). Pingamizi lolote 36 ni lazima liwekwe kwa maandishi kwa kutumia Fomu Na. 9A, na lazima litiwe saini na anayeweka pingamizi.

Uamuzi wa Pingamizi

Baada ya kupokea pingamizi, Tume itamjulisha kwa maandishi Mgombea aliyewekewa pingamizi na kumtaka atoe maelezo yake. Baada ya kupokea maelezo, Tume itatoa uamuzi wa kukubali au kukataa pingamizi husika na itawataarifu wahusika uamuzi kuhusu pingamizi hilo. Uamuzi wa Tume kuhusu pingamizi dhidi ya Mgombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais utakuwa wa mwisho.

Mgombea Pekee wa Kiti cha Rais

Kwa mujibu wa Kifungu 34 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 iwapo mgombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais aliyeteuliwa ni mmoja: -

(i) Tume itatangaza kuwa kuna mgombea pekee wa kiti cha Rais.

(ii) Tume itawasilisha jina lake kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura na itachukuliwa kuwa amechaguliwa endapo atapata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa.

(iii) Endapo mgombea huyo atashindwa kupata zaidi ya asilimia 50, Tume itapanga tarehe nyingine kwa ajili ya Uchaguzi wa Rais.