Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi yatoa ufafanuzi wanaojiandikisha zaidi ya mara moja uboreshaji wa Daftari Dar es Salaam
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imesema wakati zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linaendelea katika Mkoa wa Dar es Salaam, kumejitokeza changamoto kwa baadhi ya watu kujiandikisha zaidi ya mara moja kwenye vituo tofauti vya kuandikisha wapiga kura.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tume na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Ndg. Kailima, R.K, iwapo mtu atabainika kwamba amejiandikisha zaidi ya mara moja, taarifa zake hufutwa na mfumo katika vituo vingine na kubakizwa katika kituo cha mwisho alichojiandikisha katika Daftari. Hivyo, taarifa zaote za awali hufutwa.
Ngg. Kailima amefafanua kuwa kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 114(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, kujiandikisha zaidi ya mara moja ni kosa la jinai na akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua kiasi cha shilingi laki moja (100,000/=) na isiyozidi shilingi laki tatu (300,000/=) au kutumikia kifungo gerezani kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja, kulipa faini na kifungo gerezani.